Na marykitoto
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, ameendelea na ziara yake katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kwa lengo la kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori, kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Ziara hiyo imefanyika katika kata za Matongo, Mwantimba na Masewa ambapo wananchi walipata nafasi ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.
Katika mkutano uliofanyika kata ya Matongo, wananchi walizungumzia changamoto ya utozwaji wa fedha kwa ajili ya kumuona daktari pamoja na hali mbaya ya baadhi ya barabara zinazohitaji ukarabati wa haraka pamoja na Elimu ya uhifadhi
Akitoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya barabara, Meneja wa TARURA Wilaya ya Bariadi, Mhandisi Hussein Katakweba, alisema tayari serikali imeanza ukarabati wa barabara kuu tatu ikiwemo ya kata ya Matongo.
Alieleza kuwa barabara ya Nyawa Shuleni – Gilya – Mwauchumu yenye urefu wa kilomita sita tayari imekamilika, huku kazi ya ukarabati katika maeneo ya Mwauchumu na Salalia ikiendelea. Amesema iwapo mitambo haitapata hitilafu, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya wiki hii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndugu Khalid Mbwana, alitoa elimu kuhusu huduma za afya katika ngazi za zahanati, vituo vya afya na hospitali, hasa kuhusu gharama za kumuona daktari na matibabu kwa watoto pamoja na wajawazito.
Alieleza kuwa huduma ya kumuona daktari katika zahanati ni bure, huku gharama katika Kituo cha Afya Matongo ikiwa ni shilingi elfu mbili kutokana na sera iliyopo. Aidha, alisema gharama zinaweza kuongezeka kulingana na aina ya huduma au vipimo vinavyohitajika.
Pia alifafanua kuwa huduma za wajawazito ni bure kwa huduma za ujauzito pekee, lakini iwapo mama mjamzito atahitaji matibabu ya magonjwa mengine atalazimika kugharamia huduma hizo.
Naye Mhifadhi wa Wanyamapori wa pori la kigereshi Floravicky Kalambo Wilaya hiyo amesema ni marufuku kwa mwananchi yeyote kumiliki au kukaa na mnyama pori bila kuwa na kibali halali kutoka kwa mamlaka husika. Alisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.
Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na serikali pamoja na taasisi za uhifadhi kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na uwindaji haramu ili kulinda rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
"Alieleza kuwa uhifadhi wa wanyamapori unachangia kukuza utalii, kuongeza mapato ya serikali na kuboresha maendeleo ya wananchi kupitia miradi mbalimbali ya kijamii".
Akizungumza na wananchi, Mhe. Simon Simalenga aliwahimiza wananchi kuwa na utamaduni wa kushiriki vikao vya maendeleo na kuwauliza viongozi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanaofaulu kuingia kidato cha kwanza na kidato cha tano wanapelekwa shule kwa wakati ili kuendelea kupata elimu.
Mhe. Simalenga pia alizungumzia hatua ya serikali kujenga shule mpya ya msingi pamoja na maandalizi ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ya Matongo, hatua ambayo itapunguza umbali wa wanafunzi kufuata elimu katika maeneo ya Mwantimba na kata jirani.
Mwisho.
0 Comments