Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

BARIADI YAJIPANGA USAFI: DC SIMALENGA ATOA WITO MKALI, FAINI KWA WACHAFUZI.

 

 Mkuu wa wilaya ya bariadi             mhe.simon. Simalenga (katikati) akizungumza na wananchi 


Na marykitoto 

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, amesisitiza umuhimu wa usafi kuanzia majumbani, maeneo ya biashara na mitaro, akieleza kuwa mazingira safi ni msingi wa afya bora na maendeleo ya mji.


Akizungumza kuhusu hali ya usafi mjini Bariadi, mei 16,2026  Simalenga amesema kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama wakati wote, hasa ikizingatiwa kuwa Bariadi ni makao makuu ya Mkoa wa Simiyu.



Amesema ni muhimu wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi kila siku badala ya kusubiri kampeni maalum, akisisitiza kuwa usafi unaanzia nyumbani, maeneo ya biashara na mazingira yanayowazunguka.



Mkuu huyo wa wilaya pia ameishukuru Benki ya NMB kwa kuunga mkono juhudi za usafi kwa kuwasilisha vifaa vya usafi vitakavyosaidia kampeni hiyo. Amesema mchango huo ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuboresha mazingira.



Ameongeza kuwa anatoa wito kwa wadau wengine, taasisi na wafanyabiashara kujitokeza kusaidia upatikanaji wa vifaa vya usafi ili kuongeza nguvu katika kuhakikisha mji unakuwa safi na salama muda wote.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Idd Ndabona, amesema halmashauri tayari imeimarisha huduma za usafi kwa kuweka magari ya kuzoa taka ili kuhakikisha taka zinaondolewa kwa wakati.


Ndabona amesema halmashauri haitasita kuchukua hatua kali, ikiwemo kutoza faini kwa yeyote atakayekiuka taratibu za utunzaji mazingira. Hatua hizo zitawahusu watakaotupa taka hovyo, wanaotiririsha maji taka isivyo sahihi pamoja na wafanyabiashara watakaokaidi kushiriki au kufuata ratiba za usafi.



Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha Bariadi inakuwa mji safi, wenye mpangilio na unaovutia, sambamba na kulinda afya za wakazi wake.


Wananchi wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya mji huo unaokua kwa kasi.

Mwisho.










Post a Comment

0 Comments