Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

DAKIKA ZAGEUKA JANGA: 6 WAFARIKI, 55 WAJERUHIWA IKUNGI.

 Na marykitoto 


Safari ya abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Dodoma kuelekea Mwanza imegeuka kuwa ya majonzi baada ya ajali mbaya ya basi la Kampuni ya Greenline kutokea katika Kijiji cha Mkiwa, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Amon Kakwale, ajali hiyo ilitokea wakati basi hilo lilipojaribu kukwepa shimo barabarani. Katika jaribio hilo, dereva alishindwa kulimudu basi hilo na kusababisha kupinduka.




Tukio hilo limesababisha vifo vya watu sita papo hapo, huku wengine 55 wakijeruhiwa kwa viwango tofauti. Majeruhi wote wamekimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya haraka.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo, ikisubiri taratibu nyingine za kifamilia na kisheria.

Kamanda Kakwale amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo kamili cha ajali hiyo. Aidha, ametoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwa waangalifu wanapopita katika maeneo yenye changamoto za miundombinu.

Ajali hii imeacha simanzi kubwa kwa familia za waathirika pamoja na jamii kwa ujumla, huku ikikumbusha umuhimu wa tahadhari na uwajibikaji barabarani.



Post a Comment

0 Comments