Na marykitoto.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wanaohitimu masomo kwa kuwapa mwongozo bora wa kimaadili na kuwahimiza kuendelea na elimu ili watimize ndoto zao.
Mtanda ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 11 ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Kusekwa, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Amesema, “Wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao kielimu na kijamii, hasa wanapomaliza hatua moja ya elimu na kujiandaa kuingia hatua nyingine ya maisha.”
Aidha, amewataka wazazi kuacha kuwabagua watoto wa kike katika elimu, akisisitiza kuwa watoto wote wanastahili kupata fursa sawa za kusoma bila kujali jinsia zao.
“Ni muhimu kuwekeza katika elimu ya watoto wa kike na wa kiume kwa usawa ili kuwapa nafasi ya kutumia vipaji na uwezo wao katika kujiletea maendeleo na kulijenga taifa,” amesema.
Amewapongeza wanafunzi waliohitimu na kuwataka kuendelea kujituma, kuwa na nidhamu, kutumia muda vizuri na kutokata tamaa wanapokutana na changamoto.
Pia, amewahimiza walimu na wazazi kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi ili kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.
MWISHO.






0 Comments