Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

NEEMA NKUMBI ANG’ARA, AIBUKA MWANAHABARI BORA WA KIKE SHINYANGA 2026.



Na Kitoto Digital.

 Mwandishi wa habari Neema Nkumbi kutoka Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, ameibuka mshindi wa tuzo ya Mwanahabari Bora wa Kike (Best Female Media Personality) katika tuzo za MDAU SHUPAVU Awards 2026, Season 2.


Neema amepata tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika Oktoba 20, 2026, kwenye ukumbi wa Miligo Hall, mjini Kahama, mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika tasnia ya habari.



Mwandishi huyo ni miongoni mwa wanahabari wanaotumia majukwaa ya kidijitali kuhabarisha na kuelimisha jamii kupitia taarifa mbalimbali. Ameandika na kuchapisha habari katika majukwaa yakiwemo Huheso Digital, Meza ya Mafanikio, Udadisi Live na Malunde 1 Blog.



Ushindi huo ni ishara ya kutambua mchango wa wanawake katika tasnia ya habari, hususan katika matumizi ya majukwaa ya kidijitali yanayowezesha taarifa kuwafikia wananchi kwa haraka na kwa upana zaidi.


Tuzo za MDAU SHUPAVU Awards zimeandaliwa na Taasisi ya HOLYSMILE, chini ya Mkurugenzi wake, Arnold A. Bweichum Jr., kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa watu binafsi, taasisi na biashara zinazoshiriki katika kuleta maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali.


Tuzo hizo zinajumuisha kategoria mbalimbali, zikiwemo habari, biashara, ujasiriamali, burudani, elimu, mitindo na urembo, ubunifu pamoja na maendeleo ya jamii.



Washindi wa tuzo hizo wamepatikana kupitia mfumo wa kura za wazi, unaowapa wadau fursa ya kuonyesha chaguo lao kwa washiriki waliokuwa wakiwania tuzo hizo.


Ushindi wa Neema Nkumbi unaendelea kuonyesha nafasi muhimu ya wanahabari wanawake katika kuhabarisha umma na kutumia teknolojia ya kidijitali kuifikia jamii.

Mwisho.











Post a Comment

0 Comments