Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

BODABODA BARIADI WAPIGWA MSASA DHIDI YA UHALIFU, WATAKIWA KULINDA ABIRIA.

 



Na Kitoto Digital -Simiyu.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Chacha Maro, amewaonya waendesha bodaboda Wilaya ya Bariadi dhidi ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu, ikiwemo uporaji, ubakaji na wizi wa mali za abiria wanaowasafirisha.


(ACP) Chacha Maro, 

ACP Maro ametoa onyo hilo Oktoba 21, 2026, wakati akizungumza na waendesha bodaboda hao katika muendelezo wa kampeni ya “Ongea na Kamanda” mkoani Simiyu.


Amesema vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na baadhi ya waendesha bodaboda vinahatarisha usalama wa wananchi na kuharibu taswira ya sekta hiyo ya usafirishaji.


“Ni muhimu kwa waendesha bodaboda kuzingatia maadili ya kazi zao na kuhakikisha wanakuwa sehemu ya suluhisho la uhalifu, badala ya kujihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa wananchi,” amesema ACP Maro.


Aidha, amewataka waendesha bodaboda kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kusaidia kudhibiti vitendo hivyo katika jamii.


“Tunawaomba muendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Ushirikiano wenu ni muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yetu,” amesisitiza.


Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bariadi (OCD), Jeromino Simon, amewataka waendesha bodaboda kuzingatia sheria, kulinda usalama wa abiria wao na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika mapambano dhidi ya uhalifu.

        Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bariadi (OCD)

                                Jeromino Simon.

Amesema waendesha bodaboda wana nafasi muhimu katika kusaidia kudhibiti uhalifu kutokana na mwingiliano wao wa kila siku na wananchi katika maeneo mbalimbali.


“Tunawasihi waendesha bodaboda kuwa sehemu ya suluhisho la uhalifu kwa kutoa taarifa za mapema kuhusu vitendo vya kihalifu na watu wanaojihusisha navyo. Ushirikiano wenu ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao,” amesema.




Viongozi hao wa Jeshi la Polisi pia wamewahimiza waendesha bodaboda kuzingatia usalama barabarani kwa kuhakikisha wanavaa kofia ngumu (helmet) wao wenyewe pamoja na abiria wanaowasafirisha ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea wakati wa ajali.


Vilevile, waendesha bodaboda wametakiwa kuwasilisha kero na changamoto za kiulinzi na usalama wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku kwenye vituo vya Polisi, hususan katika kipindi hiki ambacho kampeni ya Ongea na Kamanda inaendelea.


Kampeni hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, kuwapa fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika kudumisha amani na usalama katika jamii.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments