Na marykitoto
Mahakama ya Wilaya ya Muleba imemtia hatiani Projest Tibishubwamu Frugence, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Busingo ‘B’, baada ya kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa ya Shilingi 22,500 kutoka kwa Said Nasoro Said.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAKUKURU Wilaya ya Muleba, fedha hizo zilitolewa ili kumruhusu Said Nasoro Said kuendelea kufuga mifugo katika Kijiji cha Rwanda, Kata ya Kamachumu.
Katika hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Lilian Mwambeleko (PRM), mahakama imemtaka mshtakiwa kulipa faini ya Shilingi 500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Aidha, mahakama imeamuru Shilingi 22,500 zilizohusika katika tukio hilo kurejeshwa kwa mhanga.
Baada ya kushindwa kulipa faini hiyo, Tibishubwamu amepelekwa gerezani kutumikia kifungo cha miaka mitatu.
Tibishubwamu alishtakiwa kwa kosa la rushwa kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329 (R.E. 2023).
Shauri hilo lenye namba 10966/2026 liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Wakili David Mwakyusa.
Mwisho.
0 Comments