Na marykitoto.
Septemba 18, 2026 — Wastaafu nchini wameonywa kuwa makini dhidi ya watu wanaojitambulisha kama mawakala wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), huku wakisisitizwa kutumia njia rasmi za mfuko huo kuhakiki taarifa zao na kufuatilia mafao yao ili kuepuka kuibiwa na kutapeliwa.
Tahadhari hiyo imetolewa leo mjini Shinyanga na Afisa Msimamizi wa PSSSF Mkoa wa Simiyu, Salum Mwegelo, wakati wa semina ya PSSSF kwa waandishi wa habari kutoka Klabu za Waandishi wa Habari za Shinyanga na Simiyu pamoja na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (Tanzania Bloggers Network – TBN).
Afisa Msimamizi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mkoa wa Simiyu Salum Mwegelo akizungumza.
Mwegelo amesema baadhi ya wastaafu wamekuwa katika hatari ya kupoteza mafao yao kutokana na kutumia watu wasio rasmi wanaodai kuwa wanaweza kuwasaidia katika taratibu za kuhakiki taarifa, kufuatilia au kupata mafao yao.
Amesema watu hao huwarubuni wastaafu na kuwaomba taarifa nyeti, zikiwemo namba za siri za akaunti za fedha pamoja na taarifa nyingine binafsi, ambazo zinaweza kutumiwa kufanya miamala bila ridhaa ya wahusika.
“Mawakala hao huwarubuni wastaafu na kuomba namba za siri na taarifa muhimu, ikiwemo taarifa za akaunti zao, na kisha kuzitumia kufanya miamala bila ridhaa ya wahusika na kusababisha kupoteza mafao,” amesema Mwegelo.
Mwegelo amesisitiza kuwa PSSSF haina mawakala wanaotoa huduma kwa niaba ya mfuko huo, hivyo wastaafu wanapaswa kuwa na tahadhari kubwa dhidi ya mtu yeyote anayejitambulisha kama wakala wa PSSSF na kuwaomba taarifa zao za siri.
“Usimpe mtu yeyote namba yako ya siri kwa kisingizio cha kukusaidia kupata au kufuatilia mafao yako. Tumia njia rasmi za PSSSF,” amesisitiza.
Amesema wastaafu wanapaswa kufika katika ofisi za PSSSF au kutumia mifumo rasmi ya kidijitali inayowawezesha wanachama na wastaafu kufuatilia na kuhakiki taarifa zao kwa usalama.
Kwa mujibu wa Mwegelo, matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaweza kumsaidia mwanachama kupata taarifa zake kwa urahisi bila kulazimika kumkabidhi mtu mwingine taarifa binafsi au za kifedha.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa PSSSF, Abdul Njaidi, amewataka waandishi wa habari na wanablogu kutumia taaluma yao kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu huduma za mfuko huo, hususan elimu kuhusu haki, wajibu na taratibu za kupata mafao.
Njaidi amesema vyombo vya habari, blogu na majukwaa ya kidijitali vina nafasi kubwa katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wanachama na wastaafu kwa lugha rahisi na inayoeleweka.
Aidha, amewataka waandishi na wanablogu kuthibitisha taarifa kabla ya kuzifikisha kwa umma, akisema taarifa sahihi zinaweza kusaidia wananchi kutambua njia halali za kupata huduma za PSSSF na kujilinda dhidi ya utapeli.
“Elimu sahihi ni kinga dhidi ya utapeli. Wananchi wanahitaji kujua njia sahihi za kupata huduma ili wasiwe rahisi kudanganywa na watu wasio rasmi,” amesema Njaidi.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru, amesema semina hiyo imekuwa muhimu kwa waandishi wa habari na wanablogu kwa kuwa imewaongezea uelewa kuhusu huduma za PSSSF na masuala yanayowahusu wanachama na wastaafu.
Kakuru amesema maarifa yaliyopatikana yatawasaidia waandishi na wanablogu kuandaa na kusambaza habari zenye usahihi, huku wakitoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kutumia huduma za PSSSF na kujilinda dhidi ya utapeli.
“Taarifa tulizopata hapa zitatupa uwezo wa kuandika habari zenye uelewa zaidi na kuwasaidia wananchi kujua haki zao pamoja na namna ya kujilinda dhidi ya utapeli,” amesema Kakuru.
Amesema ushirikiano kati ya PSSSF, vyombo vya habari na wanablogu ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati na kutumia huduma za hifadhi ya jamii kwa uelewa zaidi.
Aidha Mwenyekiti Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu, Paschal Michael, amewaahidi kuwa waandishi wa habari watakuwa mabalozi wazuri katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu huduma za Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Paschal amesema waandishi wana nafasi kubwa ya kuhakikisha wananchi, hususan wanachama na wastaafu, wanapata uelewa sahihi kuhusu huduma za PSSSF, haki zao pamoja na taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kupata mafao.
“Waandishi wa habari tutakuwa mabalozi wazuri wa kutoa habari na kuelimisha jamii kuhusu PSSSF, ili wananchi wawe na uelewa sahihi wa huduma zinazotolewa na mfuko na waweze kujilinda dhidi ya changamoto mbalimbali,” amesema Paschal.
Amesema kupitia habari na elimu inayotolewa na vyombo vya habari, wanachama na wastaafu wataweza kufahamu njia sahihi za kupata huduma za PSSSF na kuepuka watu wanaoweza kutumia mwanya wa ukosefu wa taarifa kuwahadaa.
Naye Mratibu wa Tanzania Bloggers Network (TBN) Kanda ya Ziwa, Kadama Malunde, amepongeza PSSSF kwa kuandaa semina hiyo, akisema mafunzo kama hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari na wanablogu kwa kuwa yanawaongezea uelewa wa masuala wanayopaswa kuyafikisha kwa jamii.
Malunde amesema waandishi na wanablogu wana wajibu wa kuhakikisha kila taarifa wanayoitoa kwa umma imethibitishwa, ni sahihi na inatoka katika vyanzo vinavyoaminika, hususan katika kipindi ambacho taarifa za kidijitali zinaweza kusambaa kwa kasi kubwa.
“Semina kama hii ni muhimu kwa sababu inatupa nafasi ya kujifunza na kuongeza uelewa. Tukiwa waandishi na wanablogu, jukumu letu si kuchapisha taarifa tu, bali kuhakikisha taarifa tunazowafikishia wananchi ni sahihi, zimehakikiwa na zina manufaa kwa jamii,” amesema Malunde.
Tahadhari iliyotolewa kwenye semina hiyo imekuja huku elimu kwa wanachama na wastaafu ikisisitizwa kuwa nyenzo muhimu ya kuwasaidia kutambua njia rasmi za kupata huduma na kuepuka kutoa taarifa zao za siri kwa watu wasiohusika.
Mwisho.
0 Comments