Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

KIJANA AJITEKA KISA SH5 MILIONI.

 


Na Mwandishi wetu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limefanikiwa kumpata kijana Gatami Maduhu Martine, mwenye umri wa miaka 20, Mkazi wa Kijiji cha Mwauchumu, Wilaya ya Bariadi, aliyeripotiwa kutoweka kwa takribani wiki moja katika mazingira ya kutatanisha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mnamo Septemba 25, 2026, majira ya saa 10:00 jioni, Polisi walipokea taarifa kutoka kwa Gatami Maduhu Maltine, mwenye umri wa miaka 64, ambaye alieleza kuwa mjukuu wake, Gatami Maduhu Martine, alikuwa ameondoka nyumbani tangu Septemba 19, 2026, akielekea katika mgodi uliopo Mwabasabi, Kata ya Gibeshi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mnamo Septemba 23, 2026, majira ya saa 4:00 usiku, kijana huyo alimpigia simu mdogo wake, Sayi Maduhu, na kudai kuwa alikuwa sehemu asiyoijua na kwamba alikuwa amefungiwa ndani ya nyumba kwa siku tano.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, watu waliodaiwa kumteka walikuwa wakidai kutumiwa kiasi cha shilingi milioni 5 ili wamuachilie.

Baada ya taarifa hiyo kufikishwa Polisi, jalada la uchunguzi lilifunguliwa katika Kituo cha Polisi Bariadi na timu ya makachero kuanza ufuatiliaji kwa kushirikiana na ndugu wa kijana huyo.

Ufuatiliaji huo ulifanikiwa kumpata Gatami akiwa Kata ya Bwanga, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, akiwa mzima wa afya na bila tatizo lolote.

Jeshi la Polisi limesema uchunguzi umebaini kuwa kijana huyo alijiteka mwenyewe kwa lengo la kupata fedha kutoka kwa ndugu zake.

Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujipatia kipato kwa njia ya udanganyifu, likieleza kuwa matukio ya aina hiyo yanaweza kusababisha taharuki katika jamii.

Polisi pia limeonya kuwa mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya aina hiyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments