Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

DC BARIADI AWAONYA NGOs: “Msikiuke Maadili, Mila na Desturi za Kitanzania”

 



Mkuu wa wilaya  Simon Simalenga akizungumza kwenye jukwaa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, amezitaka taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazofanya shughuli wilayani humo kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya Kitanzania katika utekelezaji wa miradi yao.



Simalenga ametoa kauli hiyo wakati akifungua Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) Wilaya ya Bariadi kwa mwaka 2026, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi.


Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na NGOs katika kuleta maendeleo ya wananchi, lakini amesisitiza kuwa shughuli zao zinapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.


“Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini yanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni, na kulinda mila, desturi na maadili mema ya jamii ya Kitanzania,” amesema Simalenga.



Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amezitaka NGOs kufanya kazi kwa karibu na Maafisa Maendeleo ya Jamii, ili kuwe na uelewa wa pamoja kuhusu miradi na shughuli zinazotekelezwa katika ngazi za jamii.


Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inaleta matokeo yaliyokusudiwa na inazingatia mahitaji halisi ya wananchi.


Simalenga pia amesisitiza umuhimu wa mashirika hayo kutotekeleza shughuli zao kwa kujitenga na mamlaka za serikali za eneo husika, bali kuhakikisha wadau wote muhimu wanashirikishwa katika utekelezaji wa miradi.


Mwema salum , msajili msaidizi wa NGO's Halmashauri ya mji Bariadi


Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika jukwaa hilo, Wilaya ya Bariadi ina jumla ya mashirika 35 yasiyo ya kiserikali, yanayotekeleza miradi mbalimbali katika maeneo ya elimu, afya, mazingira pamoja na uwezeshaji wananchi kiuchumi.



Mashirika hayo yamekuwa yakishiriki katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma na kuongeza fursa za maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Bariadi.


Jukwaa hilo limefanyika Septemba 28, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya shughuli wilayani humo.


Mkutano huo umetoa nafasi kwa Serikali na NGOs kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano, uwajibikaji na utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia sheria, taratibu na mahitaji ya jamii.



Licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) katika kuchangia maendeleo ya jamii na kufanikisha miradi katika sekta mbalimbali, bado yanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara unaowakwamisha kufika kwa urahisi katika maeneo wanayotekeleza miradi.


“Pamoja na mafanikio tunayoyapata katika utekelezaji wa miradi yetu, bado tunakabiliwa na changamoto ya barabara mbovu ambazo zinatufanya tushindwe kufika kwa urahisi katika baadhi ya maeneo. Hali hii wakati mwingine huathiri kasi ya utekelezaji wa shughuli zetu na kuwafikia wananchi kwa wakati,” alisema mmoja wa wawakilishi wa NGOs.

Mwisho.











Post a Comment

0 Comments