Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

EL NINO SIMIYU: JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LATOA ELIMU YA USALAMA KWA WANANCHI.

 


Na marykitoto. 

Simiyu, Septemba 1, 2026 — Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu limewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema kutokana na tishio la mvua za El Niño, ikiwemo kuzingatia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa serikali.


Akizungumza na Kitoto Digital leo Septemba 1, 2026, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Faustin Mtitu, ambaye ni Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, amesema wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema na kutopuuza taarifa rasmi kuhusu hali ya hewa.



Mtitu amesema Mkoa wa Simiyu unatakiwa kuwa makini kutokana na maeneo yake kuwa katika ukanda wa Ziwa Victoria, hususan Wilaya ya Busega, ambako baadhi ya maeneo yanaweza kuathiriwa na mvua kubwa.

Wananchi wasipuuze taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa nchi, ikiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni muhimu kuchukua tahadhari mapema,” amesema Mtitu.


Amesema wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabonde, karibu na kingo za mito, madaraja na maeneo mengine hatarishi wanapaswa kuondoka katika maeneo hayo kwa muda endapo kutakuwa na tishio, na kurejea baada ya mamlaka husika kutoa taarifa kuwa maeneo hayo ni salama.

Wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabonde, karibu na kingo za barabara, madaraja na mito wanatakiwa kuchukua tahadhari na kuhama maeneo hayo kwa muda pale kunapokuwa na tishio, hadi pale watakapotaarifiwa kuwa maeneo hayo ni salama,” amesema.


WANANCHI WATAKIWA KUKAGUA NA KUIMARISHA NYUMBA

Aidha, Mtitu amewataka wananchi kutumia muda huu kufanya ukarabati wa nyumba zao, hususan kuhakikisha paa na miundombinu mingine imeimarishwa ili kukabiliana na mvua na upepo mkali.

Pamoja na hayo, amesisitiza umuhimu wa usafi wa mazingira na kuwaonya wananchi dhidi ya kutupa taka hovyo, akisema taka zinaweza kuziba mifereji ya maji na kuongeza hatari ya mafuriko pamoja na magonjwa ya mlipuko.

Mwananchi anatakiwa kufanya ukarabati wa nyumba yake, kuhakikisha inaezekwa imara na pia kusafisha mazingira. Tusitupe taka hovyo kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuziba kwa njia za maji na hatimaye kuleta mafuriko pamoja na magonjwa ya mlipuko,” amesema.


HIFADHINI CHAKULA NA NYARAKA MUHIMU

Katika hatua nyingine, Mtitu amewashauri wananchi kuanza maandalizi mapema kwa kuhifadhi chakula cha kutosha pamoja na nyaraka muhimu katika maeneo salama ambayo hayawezi kuathiriwa na maji.

Pia amewataka wazazi na walimu kuwa makini na watoto na wanafunzi, hasa wakati wa mvua kubwa au pale tahadhari inapotolewa.

Wazazi na walimu wanapaswa kuwa makini na wanafunzi nyakati za shule. Pale tahadhari inapokuwa imetolewa, watoto wawe chini ya uangalizi na wasiachwe peke yao katika maeneo ambayo yanaweza kuwa hatarishi,” amesema Mtitu.


“USIPIME MAJI KWA MIGUU”

Jeshi hilo pia limeonya wananchi kutopima kina au nguvu ya maji kwa kutumia miguu, hasa wakati wa mafuriko, kwa kuwa maji yanaweza kuwa na kina kikubwa, mkondo mkali au hatari nyingine zisizoonekana.

Mtu yeyote asipime maji kwa miguu kwani ni hatari sana. Maji yanaweza kuwa na nguvu kubwa na kusababisha mtu kuanguka au kusombwa,” amesisitiza.


TOA TAARIFA NYAYA ZA UMEME ZILIZOANGUKA

Aidha, Mtitu amewataka wananchi kutogusa nyaya za umeme zinazoanguka wakati wa mvua au mafuriko, bali kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili hatua za usalama zichukuliwe.

Unapokuta nyaya za umeme zimeanguka, usiziguse. Toa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia namba 114 na kuwaepusha watu wengine kufika katika eneo hilo,” amesema.


Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kuwasisitiza wananchi kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa, mafuriko na majanga mengine yanayoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

Mwisho.





Post a Comment

0 Comments