Na marykitoto.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Chacha Maro, ameongoza Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali kutoka Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Simiyu kutembelea Shule ya Msingi Bethany iliyopo Wilaya ya Busega, inayotoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Ziara hiyo imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii, pamoja na kutoa faraja na msaada kwa wanafunzi hao.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, ACP Chacha Maro ameupongeza uongozi wa kituo hicho kwa juhudi kubwa unazofanya katika kuwalea na kuwahudumia watoto hao.
Amesema malezi bora na mazingira salama ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanakua katika misingi mizuri, hali inayoweza kuwasaidia kujiepusha na vitendo vya uhalifu wanapokuwa wakubwa.
“Tunawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwalea watoto hawa katika mazingira mazuri na yenye upendo. Malezi haya ni muhimu katika kuwajenga na kuwafanya wakue katika misingi inayowasaidia kuwa raia wema,” amesema ACP Maro.
ACP Maro pia amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na jamii katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kujenga uhusiano mzuri na kuimarisha usalama.
Aidha, amewataka viongozi, walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla kutosita kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale wanapobaini vitendo vya uhalifu au wahalifu, hususan vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wenye mahitaji maalum.
THE BETHANY PROJECT YASHUKURU JESHI LA POLISI
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa The Bethany Project, Jesca James Paul, ametoa shukrani za kipekee kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu kwa kutembelea kituo hicho na kuwafariji wanafunzi.
Jesca amesema kituo hicho kinaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, ikiwemo kutoa taarifa kuhusu uhalifu na wahalifu ili kusaidia kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama.
Amesema ushirikiano kati ya taasisi za malezi, jamii na Jeshi la Polisi ni muhimu katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na changamoto nyingine zinazoweza kuhatarisha ustawi wao.
WANAFUNZI WASHUKURU
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mwanafunzi Theresia Masalu ametoa shukrani kwa Jeshi la Polisi kwa msaada walioutoa, akisema umewaletea furaha na kurudisha tabasamu kwenye nyuso zao.
Ziara hiyo imeendelea kuonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kujenga mazingira salama, yenye upendo na ulinzi kwa watoto, hususan wale wenye mahitaji maalum.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kwa wakati kuhusu vitendo vya uhalifu na ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Mwisho.
0 Comments