Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YASAMBAZA MAJIKO BANIFU 122,776, YAONGEZA KASI YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

 


Na Mwandishi Wetu, Itilima

Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeendelea kuimarisha juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, ambapo hadi sasa majiko banifu 122,776 yameshasambazwa kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.



Akizungumza wakati wa semina ya utoaji elimu kwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Mtaalamu kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, Mhandisi Benezeth Kabunduguru, alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi.


"Hadi sasa Serikali imesambaza majiko banifu 122,776 kati ya lengo la majiko 200,000. Vilevile, mitungi ya gesi ya ruzuku 359,887 kati ya lengo la mitungi 452,445 tayari imesambazwa kwa wananchi ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia," alisema Mhandisi Kabunduguru.


Aliongeza kuwa pamoja na usambazaji wa majiko na mitungi ya gesi, Serikali inaendelea na hatua nyingine muhimu zikiwemo kuunganisha gesi asilia majumbani, kuhamasisha taasisi kutumia nishati safi ya kupikia na kuendesha kampeni za uelimishaji katika maeneo mbalimbali nchini.



"Mafanikio haya yanaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu. Hii itasaidia kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi," alisisitiza Mhandisi Kabunduguru.




Kwa upande wao, madiwani walioshiriki semina hiyo walieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa uelewa mpana kuhusu nafasi yao katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye maeneo wanayoyaongoza.


"Semina hii imetuongezea maarifa na imetukumbusha wajibu wetu wa kuhakikisha wananchi katika kata zetu wanapata elimu kuhusu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia. Tutaendelea kuwa mabalozi wa kampeni hii ili kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi nchini," walisema madiwani hao.



Semina hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za Serikali kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaongezeka nchini, kwa lengo la kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira na kuchochea maendeleo endelevu.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments