Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

POLISI SIMIYU WAIMARISHA UHUSIANO NA JAMII KWA VITENDO SOMANDA.

 


Na marykitoto 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limeendelea kuimarisha uhusiano na jamii kwa kutoa elimu kuhusu usalama, ulinzi na umuhimu wa kuwajali watu wenye mahitaji maalumu, huku likifanya matendo ya huruma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Somanda “A”.



Zoezi hilo limefanyika Agosti 21, 2026, katika Shule ya Msingi Somanda “A”, iliyopo Mtaa wa Bomani, Kata ya Somanda, Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu.


Katika zoezi hilo, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Asiago Ochieng, akiwaongoza maafisa wakaguzi pamoja na askari wa Usalama Barabarani Mkoa wa Simiyu, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kulinda makundi yenye mahitaji maalumu na kuhakikisha watoto wote wanakua katika mazingira salama.



Aidha, wanafunzi wamehimizwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zinazoweza kusaidia kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu, pamoja na kuzingatia elimu ya usalama barabarani.



ACP Asiago amesema kuwa kuwajali na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu ni sehemu muhimu ya kujenga jamii yenye utu, upendo, mshikamano na usawa.


Polisi ni rafiki wa kila mmoja katika jamii. Watoto wenye mahitaji maalumu wanahitaji upendo, ulinzi, heshima na mazingira salama ili waweze kutimiza ndoto zao,” alisema ACP Asiago.



Matendo hayo ya huruma yamekuwa sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu katika kuimarisha uhusiano na jamii, hasa katika kuwafikia watoto na makundi yenye uhitaji maalumu.


Jeshi la Polisi limeendelea kuhamasisha jamii kushirikiana nalo katika kulinda usalama, kuzuia uhalifu na kujenga mazingira ambayo kila mtoto, bila kujali hali yake, anaweza kusoma, kukua na kutimiza ndoto zake.

Mwisho. 







Post a Comment

0 Comments