Na marykitoto.
Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ameendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuharakisha maendeleo kwa vitendo baada ya kukabidhi mabati 212 na mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Bariadi.
Msaada huo unalenga kuimarisha miundombinu ya utawala na sekta ya elimu, huku ukitarajiwa kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Akizungumza mbele ya wananchi wakati wa ziara yake ya Kata kwa Kata, Mhandisi Kundo alisema lengo la ziara hiyo ni kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao, kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kuwaeleza vipaumbele vya Serikali kupitia Mpango wa Bajeti wa mwaka 2026/2027, huku akifafanua juu ya majukumu ya mbunge kwa wananchi.
"Ziara hii ni sehemu ya kuwashukuru wananchi, kusikiliza kero zao na kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kwa kasi ili kuboresha maisha yao, " alisema Mhandisi Kundo.
Katika ugawaji huo wa vifaa vya ujenzi, Mbunge huyo alikabidhi mabati 100 na mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Bariadi, mradi unaotarajiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, alitoa mabati 54 kwa ajili ya ukarabati wa darasa la Shule ya Msingi Kidinda lililoharibiwa na moto, hatua inayolenga kuhakikisha wanafunzi wanarejea kwenye mazingira salama na bora ya kujifunzia.
Katika kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya elimu, Mhandisi Kundo pia alikabidhi mabati 58 pamoja na mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chumba cha darasa la kompyuta katika Shule ya Sekondari Kidinda.
"Elimu ndiyo msingi wa maendeleo. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika miundombinu ya shule ili kuwapa wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia na kuwaandaa kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia," alisisitiza.
Ziara hiyo iliwakutanisha pia wataalamu kutoka idara mbalimbali za Serikali, zikiwemo Elimu, Afya, Maji, Umeme, Barabara, Ardhi, Kilimo, Mifugo na Biashara, ambao walisikiliza changamoto za wananchi na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali.
Akihitimisha mkutano huo, Mhandisi Kundo aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na kuiamini Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii na kuinua ustawi wa wananchi.
Hatua ya kukabidhi mabati na saruji imepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi wa Kata ya Bariadi, wakieleza kuwa itachochea kukamilika kwa miradi muhimu ya maendeleo na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa katika eneo hilo.
Mwisho.
0 Comments