Na marykitoto.
"Tunaishi na uchafu kila siku, hasa katika soko la jioni. Taka zimejaa na tuna hofu ya kuzuka kwa magonjwa kama hatua za haraka hazitachukuliwa."
Hayo ni malalamiko ya wakazi wa kata ya malambo, akiwasilisha kero hiyo Vaileth Nyamikenda, wakati wa mkutano wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa jimbo la bariadi mjini.
Malalamiko hayo yalimfanya Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew, kueleza kutoridhishwa na hali ya usafi katika Mji wa Bariadi, akisema bado kuna changamoto kubwa ya ukusanyaji wa taka hususan maeneo ya sokoni na mitaro ya barabara katika makao makuu ya Mkoa wa Simiyu.
Mbunge huyo aliitaka Halmashauri ya Mji wa Bariadi kubadili mfumo wa utoaji wa zabuni za usafi kwa kuwapa kipaumbele vijana na wanawake wanaowezeshwa kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
"Suala la ukusanyaji wa taka bado ni changamoto katika Mji wa Bariadi. Tenda hizi zitolewe kwa makundi maalumu. Tuwezeshe vijana na akina mama kupitia mikopo ya serikali ili wajiajiri. Taka ni fursa; tuwape vijana nafasi ya kufanya usafi ili mazingira yawe safi. Si lazima tupate mtu kutoka Arusha," alisema Mhandisi Kundo.
Mbunge huyo pia alionesha kusikitishwa na hatua ya Halmashauri kuendelea kutumia mkandarasi kutoka Arusha, akieleza kuwa changamoto ya uhaba wa vitendea kazi imekuwa ikikwamisha zoezi la ukusanyaji na uzoaji wa taka.
Kwa upande wake, Nasibu Manywele kutoka Kitengo cha Kudhibiti Taka cha Halmashauri ya Mji wa Bariadi alisema mkandarasi huyo anatarajiwa kuimarisha huduma hiyo baada ya magari matatu ya kuzoa taka kuwasili Jumatatu, Agosti 3, 2026.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Nkenyenge Charles, alikiri kuwa hali ya usafi bado hairidhishi na kwamba mji huo unahitaji maboresho ya haraka.
"Tukubali ukweli, Mji wa Bariadi bado ni mchafu. Zabuni za uzoaji taka zinatangazwa kupitia mfumo wa NeST, lakini baadhi ya waombaji huwasilisha taarifa zisizo sahihi. Wapo wanaodai wana magari mengi na wafanyakazi wa kutosha, lakini wakipewa zabuni hawaleti vifaa hivyo. Mji wetu unakua kwa kasi, hivyo robo hii tutajadili kwa kina namna bora ya kuboresha usafi wa mji," alisema Nkenyenge.
Kauli hizo zimekuja wakati wananchi wakiendelea kuitaka Halmashauri kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa taka na usafi wa mazingira, wakisisitiza kuwa mazingira safi ni msingi wa kulinda afya za wananchi na kuendana na hadhi ya Bariadi kama makao makuu ya Mkoa wa Simiyu.
Mwisho.
0 Comments