Na marykitoto
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia taaluma yao kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia, hatua itakayosaidia Serikali kufikia lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Habari MAELEZO, Bw. Rodney Mbuya, wakati akifunga Warsha ya Kuwajengea Uwezo Waandishi wa Habari na Maafisa Mawasiliano wa Serikali kuhusu Uandishi na Uhamasishaji wa Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia iliyofanyika mkoani Morogoro julai 16,2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Mbuya amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuifanya ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa moja ya vipaumbele vya kitaifa kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa miaka 10 (2024–2034).
Amesema takwimu zinaonesha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka na kufikia asilimia 28.6 ya kaya nchini, jambo linaloashiria mafanikio ya juhudi zinazoendelea. Hata hivyo, amesema bado kunahitajika kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa umma ili wananchi wengi zaidi waelewe faida za kutumia nishati safi kwa afya, mazingira na maendeleo ya uchumi.
"Vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kubadili mitazamo ya jamii. Kupitia habari, vipindi vya elimu na kampeni mbalimbali, waandishi wa habari wanaweza kuwa nguvu kubwa ya kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini," amesema Bw. Mbuya.
Aidha, amesisitiza kuwa ushiriki wa vyombo vya habari vya kitaifa na vya mikoani ni muhimu katika kuhakikisha ujumbe kuhusu nishati safi unawafikia wananchi wa maeneo yote nchini.
Katika hatua nyingine, Bw. Mbuya ameipongeza Wizara ya Nishati, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kupitia Mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, pamoja na wadau wote wa sekta ya nishati safi ya kupikia kwa kuandaa mafunzo hayo.
Amesema mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi waandishi wa habari na maafisa mawasiliano wa serikali katika kuandaa maudhui yenye ushawishi na yanayochochea wananchi kukumbatia matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Matumizi ya nishati safi ya kupikia yanachangia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kupikia, kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti, pamoja na kuboresha ustawi wa familia na kuchochea maendeleo endelevu. Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha teknolojia na huduma za nishati safi zinawafikia wananchi wengi zaidi nchini.
Kwa kuendelea kushirikiana kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na vyombo vya habari, Tanzania inaendelea kupiga hatua kuelekea kufikia lengo la matumizi makubwa ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mwisho.
0 Comments