Mkuu wa mkoa wa simiyu Mhe.Anamringi Macha.
Na marykitoto.
Wananchi wa Mkoa wa Simiyu wamehakikishiwa kuwa mkoa huo uko salama huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiwa vimejipanga kikamilifu kulinda maisha ya wananchi na mali zao wakati wote.
Hayo yamesemwa leo, Julai 6, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, alipokuwa akizungumza katika Baraza Maalum la Madiwani lililokutana kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2025/2026, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji Bariadi.
Macha amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga amani ya Mkoa wa Simiyu, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhatarisha usalama wa wananchi.
Aidha, amewataka madiwani pamoja na viongozi wa ngazi zote kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuendelea kudumisha amani, utulivu na usalama ili kuweka mazingira bora ya maendeleo ya wananchi.
Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa Mkoa pia amewahimiza wananchi kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuimarisha amani na usalama nchini, akieleza kuwa utulivu ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.
Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama wanapobaini viashiria vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali ni silaha muhimu katika kuhakikisha Mkoa wa Simiyu unaendelea kuwa salama.
Mwisho.
0 Comments