Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

RC MACHA AKAGUA UJENZI WA KITUO CHA KUPOOZEA UMEME IMALILO, ASISITIZA UKAMILIKE KWA WAKATI.

 


Na mwandishi wetu. 


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupoozea Umeme cha Imalilo kilichopo Wilaya ya Bariadi, na kueleza kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.



Mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya shilingi bilioni 8, unatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 30, 2026. Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji, hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 66.8.



Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhe. Macha ameipongeza TANESCO kwa kusimamia mradi huo kwa ufanisi na kuzingatia viwango vya ubora. Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika ndani ya muda uliopangwa ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika.


"Serikali inathamini juhudi zinazofanywa na TANESCO katika kuboresha miundombinu ya umeme. Ni muhimu kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati ili utoe huduma bora na ya uhakika kwa wananchi," amesema Mhe. Macha.



Ameeleza kuwa kukamilika kwa Kituo cha Kupoozea Umeme cha Imalilo kutaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Mkoa wa Simiyu pamoja na mikoa jirani. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuvutia uwekezaji wa viwanda, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii.



Kwa upande wake, TANESCO imehakikisha kuwa inaendelea na utekelezaji wa mradi huo kwa kasi huku ikizingatia ubora wa kazi na ratiba iliyowekwa, ili mradi ukamilike kwa wakati.


Mradi wa Kituo cha Kupoozea Umeme cha Imalilo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini. Lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme ya uhakika, endelevu na inayokidhi mahitaji ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments