Na Dawati la Habari Polisi Mwanza.
Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza (MPC) kimeungana na wadau mbalimbali kuadhimisha Siku ya Kuzuia Kuzama Maji Duniani, kikisisitiza kuwa elimu ya usalama majini, matumizi sahihi ya vifaa vya uokoaji na ushirikiano wa taasisi mbalimbali ni nguzo muhimu katika kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za majini.
Maadhimisho hayo ya kimkoa yamefanyika katika Ufukwe wa Bismarck Rock, Capri Point jijini Mwanza, yakihusisha Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wadau wengine wa usalama na wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza, Mkufunzi Mkuu wa chuo hicho, SSP Abduhaj Mkombe, alisema Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao majini, ndiyo maana limeendelea kushiriki kikamilifu katika kampeni za kuelimisha jamii kuhusu usalama wa majini.
"Sisi kama Polisi tuna dhamana ya kusimamia usalama majini na kuhakikisha raia na mali zao wanakuwa salama. Tumeona ipo haja ya kushiriki kwenye tukio hili ili kuonyesha mchango wetu katika kupunguza vifo vinavyotokana na kuzama maji," alisema SSP Mkombe.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Christopher Ngubiagai
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, aliipongeza Polisi Wanamaji pamoja na vyombo vingine vya usalama kwa ushirikiano wao katika shughuli za uokoaji na usimamizi wa usalama ndani ya Ziwa Victoria.
Alisema Serikali imeendelea kuimarisha mikakati ya kuzuia ajali za majini kwa kuboresha huduma za uokoaji na kuviwezesha vyombo vya usalama kupitia mafunzo ya mara kwa mara.
"Polisi Wanamaji na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na majanga yote ya majini wakati wowote," alisisitiza Ngubiagai.
Kwa upande wake, ASP Prisca Lawei, aliyemwakilisha Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, alisema jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa wavuvi na wananchi wanaoishi kandokando ya Ziwa Victoria kuhusu namna ya kujikinga na kujinusuru pale ajali za majini zinapotokea.
Alieleza kuwa uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya vifaa vya kuokoa maisha pamoja na kufuata tahadhari zote za usalama unapunguza kwa kiwango kikubwa madhara yanayotokana na ajali za majini.
Naye Polisi Kata wa Kata ya Nyamagana, Mkaguzi wa Polisi Luhendeka Masanja, alisema eneo la Bismarck Rock ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa na watalii na wananchi wengi, hivyo elimu ya usafiri salama imeendelea kutolewa ili kuhakikisha kila mtumiaji wa eneo hilo anazingatia kanuni za usalama.
Maadhimisho hayo yamekuwa sehemu ya kuhamasisha jamii kutambua kuwa ajali nyingi za majini zinaweza kuzuilika endapo wananchi watazingatia sheria za usalama, kutumia vifaa vya kuokoa maisha na kufuata maelekezo ya wataalamu wa usalama majini.
Mwisho.
0 Comments