Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI SALOME MAKAMBA AFUNGUA WARSHA YA NISHATI SAFI MOROGORO.

 


Na marykitoto. 

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amefungua warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari pamoja na Maafisa Mawasiliano wa Serikali kuhusu uandishi na uhamasishaji wa masuala ya Nishati Safi ya Kupikia, iliyofanyika katika Ukumbi wa Morena Hotel, mkoani Morogoro.



Katika hafla hiyo, Mhe. Makamba aliwasili akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, ambapo walipokelewa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati pamoja na wadau wa maendeleo.



Warsha hiyo imeandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), kupitia Mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya. Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha waandishi wa habari na Maafisa Mawasiliano wa Serikali kuandika kwa weledi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa manufaa ya afya, mazingira na maendeleo ya jamii.



Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo, Mhe. Salome Makamba alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari na wataalamu wa mawasiliano katika kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi kuhusu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia na mchango wake katika kulinda mazingira, kuboresha afya za wananchi na kuharakisha maendeleo endelevu.



Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliambatana na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia wa Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Nishati, Bi. Nteghenjwa Hosseah, pamoja na Meneja wa Mradi wa CookFund–UNCDF, Bw. Imanuel Muro.



Warsha hiyo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Nishati na wadau wake katika kuimarisha uelewa wa umma kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, sambamba na kuunga mkono ajenda ya taifa ya kuongeza matumizi ya nishati safi kwa wananchi.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments