Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

ENG. KUNDO AANZA ZIARA YA MAENDELEO ISANGA, SARUJI, PAMPU NA MABATI VYATOLEWA KWA USTAWI WA WANANCHI.

 


Na marykitoto. 

Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, julai 20, 2026 ameanza ziara ya kutembelea kata mbalimbali kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi, huku akikabidhi vifaa mbalimbali vya maendeleo katika Kata ya Isanga, Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu. 


Katika ziara hiyo, Eng. Kundo alikabidhi mifuko 430 ya saruji, pampu 17 za maji na mabati 104 kwa ajili ya kuimarisha sekta za elimu na upatikanaji wa maji safi na salama.



Akizungumza na wananchi, Mbunge huyo alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za maji, elimu, barabara na umeme, akisema hatua hizo zimeendelea kuboresha maisha ya wananchi wa Jimbo la Bariadi Mjini.

Mgao wa Vifaa vya Elimu

Eng. Kundo alieleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kukamilisha na kuboresha miundombinu ya shule mbalimbali katika Kata ya Isanga.

Mgao wa saruji ulikuwa kama ifuatavyo:

Shule ya Msingi Isanga A – mifuko 100 ya saruji na mabati 104.

Shule ya Msingi Isanga C – mifuko 100 ya saruji.

Shule ya Sekondari Katenga – mifuko 200 ya saruji.

Shule ya Msingi Majahida – mifuko 30 ya saruji.

Aidha, alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Mwatungu kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 304, hatua inayolenga kupunguza umbali wa kutembea kwa wanafunzi kufuata huduma za elimu.



Pampu 17 Kuboresha Huduma ya Maji

Katika sekta ya maji, Mbunge huyo alikabidhi pampu 17 zitakazofungwa kwenye visima vya maji kupitia mpango wa dharura, ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Kata ya Isanga.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bariadi (BARUWASA), Mhandisi Nhandi Mathias, alisema Serikali imetoa Shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji katika kata hiyo.


Alieleza kuwa fedha hizo zitatumika kujenga tenki la maji pamoja na kutandaza mabomba yenye urefu wa takribani kilomita 25, huku mradi ukitarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.


Aliongeza kuwa maeneo ya Londo na Wala yatanufaika na mradi huo, huku pampu zilizotolewa zikitarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.


Umeme na Barabara Vyatajwa Kuwa Kipaumbele

Eng. Kundo alisema Halmashauri ya Mji wa Bariadi ina mitaa 92, ambapo tathmini imeonyesha kuwa baadhi ya maeneo ya mjini bado yana hali inayofanana na vijijini.


Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali imewasilisha mitaa 63 kwenye mpango wa kuunganishiwa umeme kwa gharama nafuu ya Shilingi 27,000 kwa kila mwananchi anayestahili.

Wananchi Wawasilisha Kero

Katika mkutano huo, wananchi waliomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na kufikisha huduma ya umeme katika Shule ya Sekondari Katenga ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.


Mkazi wa Majahida, Limi Silanga, aliomba pia Serikali kuharakisha utatuzi wa migogoro ya ardhi na upimaji wa viwanja ili wananchi waweze kumilikishwa maeneo yao na kunufaika na huduma mbalimbali za kifedha, ikiwemo mikopo.


Akihitimisha ziara yake ya kwanza katika Kata ya Isanga, Eng. Kundo aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kuahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wakazi wa Bariadi Mjini.

 MWISHO.

Post a Comment

0 Comments