Na marykitoto.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa jamii kwa kuyafikia makundi mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uelewa kuhusu usalama, amani na uwajibikaji katika jamii.
Akizungumza kupitia usalama kwanza Jogging ( kata wese ) Mkaguzi wa Polisi kata ya somanda Mwinjuma Omary amewahimiza vijana kuendelea kuwa walinzi wa amani kwa kuepuka kujihusisha na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani katika jamii. Amesema kuwa vijana wana nafasi kubwa katika maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kutumia nguvu na uwezo wao katika shughuli zenye tija badala ya kushiriki katika matendo yanayokiuka sheria.
Mbali na hilo, Mkaguzi Omary ametoa wito kwa vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya na yenye manufaa. Ameeleza kuwa mitandao inaweza kuwa chombo muhimu cha kujifunza, kuwasiliana na kuendeleza shughuli za kijamii na kiuchumi, lakini matumizi mabaya yanaweza kusababisha migogoro, chuki na hata kuvunja amani katika jamii.
“Vijana wanapaswa kuepuka kutumia mitandao ya kijamii kama majukwaa ya kutoa lugha zisizo na staha au zinazoweza kuleta taharuki kwa watu wengine. Badala yake, watumie teknolojia hiyo kuelimishana, kubadilishana mawazo ya maendeleo na kujenga mshikamano,” alisema Mkaguzi Omary.
Rai hiyo ilitolewa Juni 20, 2026, mara baada ya mazoezi ya kikundi cha Usalama Kwanza Jogging Clubs kilichopo Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu. Tukio hilo lilitoa fursa kwa Jeshi la Polisi kuzungumza na vijana na wanachama wa kikundi hicho kuhusu umuhimu wa kulinda amani na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limeendelea kusisitiza ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama, likiamini kuwa elimu ya mara kwa mara ni nyenzo muhimu katika kuzuia uhalifu na kuimarisha utulivu wa jamii.
Mwisho.
0 Comments