Na Beda Msimbe, St. Petersburg, Urusi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza mkakati mpya wa kuimarisha sekta ya utalii kwa kulenga soko kubwa la Urusi, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.
Akizungumza katika St. Petersburg International Economic Forum 2026 uliofanyika Juni 5, 2026 mjini Saint Petersburg, Rais Samia alisema ushirikiano wa miaka 65 wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi sasa unaingia katika hatua mpya inayolenga kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.
Rais Samia alibainisha kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kulitumia soko la Urusi, ambalo lina idadi kubwa ya watalii wanaosafiri katika maeneo mbalimbali duniani kila mwaka. Alisema Serikali imeanza kuondoa baadhi ya vikwazo vilivyokuwa vikikwamisha ukuaji wa soko hilo, ikiwemo kuboresha upatikanaji wa safari za ndege kati ya nchi hizo mbili.
Katika hatua muhimu ya kuimarisha sekta ya utalii, Rais Samia alitangaza kuwa kuanzia Julai 2, 2026, Air Tanzania itaanza safari za moja kwa moja zinazounganisha Dar es Salaam, Moscow na Zanzibar.
Alieleza kuwa huduma hiyo mpya ya usafiri wa anga itarahisisha safari kwa watalii wa Urusi wanaotaka kutembelea Tanzania na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa. Serikali inalenga kufikisha idadi ya watalii kutoka Urusi hadi 500,000 ifikapo mwaka 2030, huku lengo la muda mrefu likiwa kufikia watalii milioni moja.
Aidha, Rais Samia alieleza kuwa jitihada za kuitangaza Tanzania kimataifa zinaungwa mkono na mafanikio mbalimbali ambayo nchi imeendelea kuyapata katika sekta ya utalii. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kutambuliwa kwa Serengeti National Park kama hifadhi bora zaidi barani Afrika, pamoja na Zanzibar kuendelea kupata sifa kama moja ya maeneo bora kwa mikutano, utalii na mapumziko.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia alisisitiza kuwa dunia inabadilika kwa kasi na kwamba mataifa ya Afrika yako tayari kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia kupitia mifumo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo African Continental Free Trade Area. Alisema Tanzania imefungua milango kwa wawekezaji, wabunifu na wafanyabiashara kutoka duniani kote kushiriki katika fursa mpya za maendeleo na ukuaji wa uchumi.
"Tanzania iko tayari kwa hatua mpya ya maendeleo. Tunakaribisha ushirikiano, uwekezaji na ubunifu kutoka kwa wadau wote wanaotaka kuwa sehemu ya safari yetu ya mabadiliko," alisisitiza Rais Samia.
Tangazo la kuanza kwa safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na Urusi linaashiria hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili na kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na utalii. Kwa kutumia nguvu ya vivutio vyake vya kipekee na kuboresha miundombinu ya usafiri, Tanzania inaendelea kujijengea nafasi kubwa katika soko la utalii la kimataifa.
Mwisho.
0 Comments