Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

RC MACHA AKEMEA RUSHWA, ATAKA TEKNOLOJIA IRAHISISHE HUDUMA KWA WANANCHI.




Na marykitoto. 

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mkoa wa Simiyu umeendesha semina kwa waajiri pamoja na maafisa wanaoshughulikia masuala ya wanachama, kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma na kuongeza uelewa kuhusu mifumo ya hifadhi ya jamii.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Meneja wa PSSSF Mkoa wa Simiyu, Salum Mwegero, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora kwa wakati.

Meneja wa PSSSF Mkoa wa Simiyu, Salum Mwegero 

Mgeni rasmi wa semina hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema dunia ya sasa inaendeshwa na teknolojia ya kidijitali, jambo linalowezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi popote walipo.


"Amesisitiza kuwa mifumo ya kidijitali inapaswa kuwa rafiki kwa watumiaji na isiwe chanzo cha usumbufu kwa walengwa wa huduma. Amesema Mhe.Macha "

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anamringi Macha mgeni rasmi 

Mhe. Macha pia ametoa rai kwa taasisi na wadau kuhakikisha elimu kuhusu huduma mbalimbali inatolewa mapema kwa wananchi ili kusaidia kutatua changamoto zinazojitokeza, hususan zile zinazohusiana na tofauti za majina katika vitambulisho na nyaraka mbalimbali muhimu.



Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amekemea vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, uwajibikaji na haki kwa wanachama wote wanaohudumiwa na taasisi za umma.


Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wamepongeza mafunzo hayo wakisema yamewapa uelewa mpana zaidi kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma.


 Pia wameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na mgeni rasmi ili kuboresha huduma kwa wanachama wa PSSSF katika maeneo yao ya kazi.




Semina hiyo ni sehemu ya juhudi za PSSSF za kuendelea kuimarisha ushirikiano na waajiri pamoja na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora, za haraka na zenye kuzingatia mahitaji ya wakati wa sasa.

Mwisho.















Post a Comment

0 Comments