Na Dawati la Habari Polisi Mwanza.
Wananchi wa Kata ya Buhongwa pamoja na kata jirani ya Lwanhima katika Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, wameonyesha mshikamano wa kipekee kwa kuanzisha juhudi za kukijenga upya Kituo cha Polisi Buhongwa kilichoharibiwa kwa moto wakati wa vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi kukumbana na changamoto kubwa ya kupata huduma za kipolisi, hali iliyowalazimu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana karibu nao. Kabla ya kuharibiwa, kituo hicho kilikuwa kinahudumia zaidi ya wananchi 200,000 kutoka kata za Buhongwa, Lwanhima na Mkolani.
Akizungumza mbele ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 22, 2026, Diwani wa Kata ya Buhongwa, Mhandisi Anderson Mfinanga, alisema vijana waliohusika na tukio la uchomaji wa kituo hicho wamejifunza kutokana na madhara yaliyotokea na sasa wameonyesha utayari wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kurejesha huduma hiyo muhimu.
"Kwa mateso tuliyopitia tangu kituo chetu kilipochomwa moto, sasa wamesema mateso yatosha na wako tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi kurejesha huduma," alisema Mfinanga.
Diwani huyo alieleza kuwa wananchi tayari wameanza kuchangia vifaa vya ujenzi na malighafi mbalimbali ili kuhakikisha ujenzi unaanza haraka na huduma za usalama zinarejea katika eneo hilo.
Katika mkutano huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, alikubali ombi la wananchi la kujenga upya kituo hicho kwa nguvu zao wenyewe, huku akiwataka kujifunza kutokana na yaliyotokea na kuhakikisha matukio ya vurugu hayajirudii tena.
"Tunawasamehe, lakini ni muhimu kutafakari kwa kina ni nini kilisababisha kufikia hatua ya kuchoma kituo cha polisi pamoja na mali nyingine za serikali na watu binafsi," alisema Kamanda Mutafungwa.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila mazingira salama na yenye mshikamano.
Juhudi za kurejesha kituo hicho zimeungwa mkono na makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo wafanyabiashara ambao wanasema wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kukosekana kwa huduma za usalama karibu na maeneo yao.
"Hata sisi wafanyabiashara tumepata adha kubwa tangu kituo hiki kilipochomwa moto. Tunahitaji huduma hii irejee haraka," alisema Mahiri Chacha, mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo.
Kwa upande wake, mkazi wa Buhongwa, Zaidi Harub, alisema tukio hilo limewaacha wananchi katika hali ya hofu kwa muda mrefu na kuwataka wote kujifunza kutokana na makosa ya nyuma.
Katika hatua ya kuonyesha dhamira ya kweli ya kurejesha huduma hiyo, wananchi walichangia zaidi ya shilingi milioni 5 taslimu, mifuko 74 ya saruji pamoja na matofali 1,200 wakati wa mkutano huo. Makadirio yanaonyesha kuwa zaidi ya shilingi milioni 30 zinahitajika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.
Jitihada hizi zinaonekana kuwa ishara ya umoja, maridhiano na utayari wa wananchi kushiriki moja kwa moja katika maendeleo ya jamii yao pamoja na kuimarisha usalama katika eneo la Buhongwa.
Mwisho.
0 Comments