Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

JENEZA DOGO LAZUA TAHARUKI MAGU, POLISI WAENDELEA NA UCHUNGUZI.



Na mwandishi wetu. 

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea na uchunguzi wa tukio la kuonekana kwa jeneza dogo lililotelekezwa katika uwanja wa Soko la Mnada la Kabila, lililopo Kata ya Kabila, Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza.


Akizungumza na waandishi wa habari Juni 29, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa, alisema kuwa majira ya saa 11:00 alfajiri Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu uwepo wa jeneza hilo katika eneo la soko.


Alisema mara baada ya kupokea taarifa hiyo, askari walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi. Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa jeneza hilo lilikuwa na rangi ya zambarau na lilikuwa na msalaba wa rangi nyeupe.


Kwa mujibu wa DCP Mutafungwa, ndani ya jeneza hilo walikuta vipande vya nyama, kichwa na miguu ya kondoo pamoja na vitu vinavyodhaniwa kuwa dawa za kienyeji.


Kamanda huyo amesema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kubaini waliohusika na sababu za kuacha jeneza hilo katika eneo la soko.


Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Magu na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu, kuepuka kueneza taarifa zisizo na uthibitisho, na kutokuwa na imani potofu za kishirikina zinazoweza kusababisha taharuki au kuwafanya kuwashutumu na kuwadhuru watu wengine bila ushahidi.


Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa litawafikisha mbele ya sheria wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo mara uchunguzi utakapokamilika.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments