Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limekamata jumla ya watuhumiwa 642 wa makosa mbalimbali ya jinai katika operesheni maalum za misako zinazoendelea katika maeneo tofauti ya mkoa huo, kuanzia Mei 1, 2026 hadi sasa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, hali ya usalama katika mkoa huo ni shwari, huku jeshi hilo likiendelea kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao kupitia doria na misako ya mara kwa mara.
Mafanikio ya Misako ya Polisi
Katika operesheni hizo, watuhumiwa 97 walikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na pombe haramu ya moshi (gongo), watuhumiwa 5 wakikamatwa wakiwa na zana haramu za uvuvi, 158 wakihusishwa na kucheza kamari, huku 261 wakikamatwa wakiwa na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi.
Aidha, watuhumiwa 5 wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji, wakati wengine 116 wakikamatwa kuhusiana na dawa za kulevya ambapo kiasi cha bangi kilo 9 pamoja na misokoto 329 vilikamatwa.
Vielelezo vingine vilivyokamatwa ni pamoja na televisheni 10, kompyuta mpakato 3, simu 8, pikipiki 19, magunia 3 ya mpunga, pamoja na vifaa mbalimbali vya nyumbani na vya uhalifu kama vile vifaa vya kuvunjia nyumba.
Watuhumiwa 5 wa Mauaji Misungwi
Polisi pia wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 5 wanaohusishwa na mauaji ya Mariam Faya Nduta (38), mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Mwesengi, Wilaya ya Misungwi.
Tukio hilo lilitokea Aprili 16, 2026 majira ya saa 1:40 usiku, ambapo marehemu aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mgongoni.
Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo kuwa ni mgogoro wa ardhi.
Watuhumiwa waliokamatwa ni:
Shilinde Lucas Kisusi (24)
Nicholaus Leonard Andrea (37)
Lucas Joseph Lutandika (46)
Mathias Paulo Lutandika (50)
Mping’wa Faya Nduta (62)
Watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na watachukuliwa hatua za kisheria.
Watuhumiwa Wawili Kufikishwa Mahakamani
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha mahakamani watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya kijana Mzafaru Faisal Yunus yaliyotokea katika baa ya Las Vegas, Wilaya ya Ilemela.
Watuhumiwa hao ni Yohana Paul Peter (22), aliyekuwa mlinzi katika eneo la tukio, na Hamis Juma Musa (27), mfanyakazi wa usafi wa baa hiyo. Wamesomewa shtaka la mauaji namba 10492 ya mwaka 2026.
Jeshi la Polisi limewashukuru wananchi kwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu, hatua ambayo imechangia mafanikio ya operesheni hizo na kusaidia kudhibiti uhalifu.
Polisi wamesema wataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wananchi kuhakikisha usalama unaimarika zaidi katika Mkoa wa Mwanza.
#Mwanza #PolisiTanzania #Uhalifu #Misako #Usalama #TanzaniaNews
Mwisho.
0 Comments