Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

USALAMA KWANZA JOGGING CLUB #KATAWESE YAZIDI KUNG’ARA; WANACHAMA 15 WAPYA WAJIUNGA KWA KISHINDO.

 


Na marykitoto 

Harakati za kuhamasisha afya na mshikamano wa kijamii kupitia mazoezi zinazidi kushika kasi katika Kata ya Somanda, Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, ambapo usalama kwanza Jogging Club (KATA wese) imeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii.


Mbali na kufanya mazoezi ya pamoja kila wiki, klabu hiyo imekuwa mstari wa mbele katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira mjini Bariadi pamoja na kusaidiana katika nyakati za shida na furaha miongoni mwa wanachama wake.


Safari ya jogging ya mei 9  ilianzia katika Shule ya Msingi Somanda, ikipitia barabara kuu ya Nyerere Road hadi njia panda ya Muungano, huku wanachama wakizunguka maeneo mbalimbali ya mji wa Bariadi katika kata za Malambo, Sima na Bariadi kabla ya kurejea tena Somanda ambapo walihitimisha zoezi hilo katika Shule ya Msingi Somanda.





Kwa mujibu wa waandaaji, safari hiyo ilikuwa na umbali wa zaidi ya kilomita 11, jambo lililoonyesha hali kubwa ya wanachama katika kuimarisha afya zao pamoja na kuendeleza umoja ndani ya jamii.


Moja ya mambo yaliyogusa mioyo ya wengi katika mkusanyiko huo ni taarifa ya msiba wa baba mzazi wa mmoja wa wanachama wa klabu hiyo, ambapo wanachama walijadili namna bora ya kushiriki na kutoa faraja kwa mwenzao katika kipindi hicho kigumu.


Katika hatua nyingine ya kufurahisha, klabu hiyo imepokea wanachama wapya 15 waliojiunga rasmi na familia ya “Wakata Wese” wa Mkoa wa Simiyu, hatua inayodhihirisha ukuaji mkubwa wa klabu hiyo na mvuto wake kwa jamii.



Usalama kwanza Jogging Club inaendelea kuthibitisha kuwa mazoezi siyo tu njia ya kujenga afya, bali pia ni daraja la kuimarisha upendo, mshikamano na maendeleo ya jamii.

Mwisho.



Post a Comment

0 Comments