Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

TPF–NET YAWAINUA POLISI WANAWAKE SIMIYU KITAALUMA.

 


Na mwandishi wetu. 

Wanachama wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF–Net) mkoani Simiyu wamepatiwa mafunzo maalumu yaliyolenga kuimarisha weledi, maadili ya kazi na utoaji wa huduma bora kwa jamii. 


Mafunzo hayo yalitolewa na Katibu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF–Net), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pili Mande, aliyekuwa ameambatana na Mkaguzi wa Polisi Wilfred Willa.



Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, SACP Pili Mande aliwataka askari wanawake kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.



 Alisisitiza kuwa askari wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya Jeshi la Polisi na wanapaswa kujituma, kuwajibika na kujitoa kikamilifu katika kazi zao za kila siku.



Aidha, SACP Mande alieleza kuwa nidhamu, uadilifu na uzingatiaji wa maadili ya kazi ni nguzo muhimu zinazosaidia kujenga taswira chanya ya Jeshi la Polisi mbele ya jamii. 

Aliwahimiza wanachama wa TPF–Net kutumia elimu hiyo kama chachu ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.



Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Edith Swebe, aliwaongoza maafisa, wakaguzi pamoja na askari wa vyeo mbalimbali kushiriki na kupokea mafunzo hayo. Alitoa shukrani kwa viongozi wa TPF–Net kwa kutembelea mkoa huo na kutoa elimu yenye manufaa makubwa kwa askari wanawake.



ACP Swebe alisema mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwa washiriki, kwani yameongeza uelewa kuhusu wajibu wao wa kazi, umuhimu wa maadili ya utumishi na namna bora ya kuhudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.


Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF–Net) za kuendelea kuwawezesha askari wanawake kitaaluma na kiutendaji, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ubora na kuchangia katika kuimarisha usalama na amani nchini.

Mwisho.










Post a Comment

0 Comments