Na marykitoto.
Mamia ya wanafunzi wa shule za msingi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Simiyu Mei 30, 2026 wamekutana wilayani Maswa kwa ajili ya kambi maalum ya maandalizi ya mashindano ya UMITASHUMITA ngazi ya mkoa, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea mashindano ya kitaifa yatakayofanyika mkoani Iringa.
Akiwasilisha taarifa ya ufunguzi wa mashindano hayo ya UMITASHUMITA 2026 ngazi ya mkoa, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi – Elimu Ester Marwa alisema mashindano hayo yanalenga kuibua na kukuza vipaji mbalimbali vya wanafunzi kupitia michezo na sanaa.
Alieleza kuwa jumla ya wanafunzi 817 wanashiriki kambi ya maandalizi iliyoanza Mei 30 hadi Juni 1, kisha kufuatiwa na mashindano ya ngazi ya mkoa yatakayofanyika Juni 11 hadi 13.
Baada ya mashindano hayo, watachaguliwa wanafunzi 120 watakaoiwakilisha Simiyu katika mashindano ya taifa yatakayofanyika Iringa kuanzia Juni 7 hadi 18, 2026, chini ya kauli mbiu isemayo: “Michezo na sanaa shuleni ni daraja la ajira, afya na ushindani wa kimataifa.”
Akizindua kambi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anamringi Macha aliwapongeza wanafunzi, walimu na viongozi wote wanaosimamia michezo kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto.
Alisisitiza umuhimu wa nidhamu, uadilifu na upendo miongoni mwa wanafunzi, akieleza kuwa misingi hiyo ndiyo msingi wa mafanikio katika michezo na maisha kwa ujumla.
Aidha aliwataka walimu kuhakikisha mwanafunzi yeyote asiye na nidhamu au upendo arudishwe nyumbani na asiruhusiwe kuendelea na michezo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu Bi. Prisca Kayombo amewataka wanafunzi kutumia fursa hiyo kujifunza zaidi kutoka kwa wenzao na kuimarisha ujuzi wao. Pia amesisitiza walimu kudumisha nidhamu wakati wote na kuhakikisha washiriki wanashindana kwa haki na kurejea na ushindi.
Kwa upande wake, Mwalimu Aziz Abedy kutoka Halmashauri ya Mji Bariadi amesema walimu wamepewa dhamana ya kuwalinda na kuwalea wanafunzi hao katika michezo, na wako tayari kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na uongozi wa mkoa.
Aidha amewahimiza wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki michezo kwani ni njia muhimu ya kujenga vipaji na fursa za ajira za baadaye.
Wanafunzi washiriki wa kambi hiyo wameahidi kudumisha nidhamu, upendo na bidii kama walivyoelekezwa na viongozi wao, na wamesema wamejipanga kufanya vizuri katika mashindano hayo na kurejea na makombe kwa heshima ya Mkoa wa Simiyu.
Uzinduzi huo ulipambwa kwa shamrashamra mbalimbali zilizovutia washiriki na wageni waalikwa, ambapo michezo mbalimbali ilionekana kushika kasi ikijumuisha mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa mikono, riadha pamoja na kujibu maswali ya papo kwa papo na kuimba, huku kila mchezo ukionyesha ushindani na vipaji vya hali ya juu vya wanafunzi.
Aidha, burudani ya ngoma za asili kutoka kwa vikundi vya wanafunzi ilipamba shughuli hiyo, ikiongeza hamasa na kuonesha utajiri wa utamaduni wa Mkoa wa Simiyu kupitia midundo, nyimbo na vigelegele vilivyovutia watazamaji wengi.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anamringi Macha, alizindua rasmi kambi hiyo kwa tukio la kuvutia la kupiga penalti, hatua iliyopokelewa kwa shangwe kubwa na wanafunzi, walimu na wananchi waliohudhuria. Tukio hilo liliashiria uzinduzi rasmi wa maandalizi hayo na kuongeza hamasa kwa washiriki kuelekea mashindano ya mkoa na hatimaye kitaifa.
Kwa ujumla, uzinduzi huo umeweka mazingira mazuri ya maandalizi ya UMITASHUMITA 2026, huku ukisisitiza umuhimu wa michezo na sanaa kama chachu ya kukuza vipaji, nidhamu na mshikamano miongoni mwa wanafunzi wa Mkoa wa Simiyu.
Mwisho.

0 Comments