Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

MAAFISA MAENDELEO BUSEGA WAKABIDHIWA PIKIPIKI KUIMARISHA HUDUMA KWA WANANCHI WA VIJIJINI.

 



Na mwandishi wetu. 

Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu Region wamekabidhiwa pikipiki kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao na kuongeza ufanisi wa kuwafikia wananchi, hususan wa maeneo ya vijijini, kwa wakati.


Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mkuu wa Wilaya hiyo, Faidha Salimu aliwataka maafisa hao kutumia vitendea kazi hivyo kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha wanawafikia wananchi wa vijijini kwa karibu zaidi.



Mhe. Salimu pia aliwasisitiza kwenda kutoa elimu kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali bila riba kupitia mapato ya ndani ya halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Alisema wananchi wanapaswa kuhamasishwa kuunda vikundi na kuomba mikopo hiyo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza miradi ya ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi.


Aidha, aliwataka maafisa hao kuwaelimisha wananchi kujiepusha na mikopo umiza maarufu kama “kausha damu” na badala yake kutumia huduma za taasisi za kifedha zinazotambulika na serikali.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Hamidu Hamisi alisema halmashauri itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma kwa kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.



Aliongeza kuwa Idara ya Maendeleo ya Jamii ina mchango mkubwa katika kufanikisha maendeleo endelevu, hivyo maafisa hao wanapaswa kuwahudumia wananchi kwa weledi na kujituma.


Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Busega, Flora Barakana amesema pikipiki hizo zimegharimu zaidi ya shilingi milioni 62, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.



Flora alibainisha pia kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Busega imetoa zaidi ya shilingi milioni 586 kama mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 hadi Machi 2025/2026, ikiwa ni mkakati wa kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia shughuli za maendeleo na ujasiriamali.

Mwisho. 






Post a Comment

0 Comments