Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

KUTOKA SH500 HADI SH1,000: NAULI ZA ‘DALADALA’ ZAWAUMIZA WANANCHI SIMIYU.




Na marykitoto 

Katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Simiyu , kumekuwa na ongezeko la nauli za baiskeli zinazotumika kama usafiri wa abiria maarufu “daladala”, ambapo safari zilizokuwa zikitozwa Sh500 sasa zimefikia Sh1,000.


Mabadiliko hayo yameripotiwa zaidi katika wilaya za Maswa, Bariadi na Meatu, huku wananchi wengi wakisema hali hiyo imeongeza ugumu wa maisha kwa watu wa kipato cha chini wanaotegemea usafiri huo kila siku.


Baadhi ya wakazi wameeleza kuwa ongezeko hilo linaathiri shughuli zao za kila siku ikiwemo kwenda sokoni, kazini na kufanya biashara ndogo ndogo, huku wengine wakilazimika kutembea umbali mrefu ili kupunguza matumizi ya usafiri.


Waendesha baiskeli za kubeba abiria maarufu daladala wakiwa wanasubiri abiria katika moja ya vituo vyao mjini Bariadi. 


Kwa upande wao, baadhi ya watoa huduma wa usafiri huo wanasema kupanda kwa nauli kunachangiwa na hali ngumu ya uchumi pamoja na kuongezeka kwa gharama za maisha na matengenezo ya baiskeli.



Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa hali hiyo ni sehemu ya mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo gharama za huduma na bidhaa zimekuwa zikiongezeka kutokana na kupanda kwa mahitaji ya maisha ya kila siku.


Hata hivyo, wananchi wameiomba serikali pamoja na mamlaka husika kufuatilia hali hiyo ili kuhakikisha gharama za usafiri zinaendelea kuwa rafiki kwa wananchi wa kawaida.

Mwisho. 


Una maoni gani ....................

Post a Comment

0 Comments