Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

KAMANDA SWEBE ATETA NA WAZEE BARIADI KATIKA ZIARA YA MTAA KWA MTAA.



         Kamanda Swebe akiteta na wazee          wa mji wa zamani Bariadi.

Na marykitoto. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Edith Swebe, ameanza ziara ya mtaa kwa mtaa kwa kukutana na wazee wa Mji wa Zamani uliopo Mtaa wa Bariadi, ambapo amesisitiza umuhimu wa malezi bora kwa vijana ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili na vitendo vya uhalifu.



Akizungumza na wazee hao katika kijiwe cha kahawa maarufu cha Mzee Majebele, Kamanda Swebe amewataka wazee kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa malezi na maadili mema kwa vijana, akieleza kuwa wazee wana nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye uzalendo na amani.


Amesema kuwa ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi ni muhimu katika kuzuia na kupambana na uhalifu, hivyo amewahimiza wazee kutoa taarifa za wahalifu na viashiria vya uhalifu mapema ili hatua zichukuliwe kwa wakati.


Aidha, Kamanda Swebe amewataka wazee hao kujitokeza kupima magonjwa yasiyoambukiza katika Kituo cha Afya cha Polisi, na ameahidi kuwa Jeshi la Polisi litagharamia vipimo hivyo kwa wazee wa eneo hilo.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bariadi, Saidi Mapesa, amempongeza Kamanda Swebe kwa ukaribu wake na wananchi, hususan kwa kuwatembelea wazee na kuzungumza nao moja kwa moja katika kijiwe chao cha kahawa.


Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kubaini, kuzuia na kutanzua viashiria vya uhalifu mapema.


Kamanda Swebe alifanya ziara hiyo leo Mei 13, 2026, ambapo pia alitangazwa kuwa mlezi wa kijiwe hicho cha wazee wa Mtaa wa Bariadi.

Mwisho.








Post a Comment

0 Comments