Na marykitoto
Wilaya ya Bariadi imeshuhudia tukio kubwa na la kuvutia la utamaduni baada ya Maelfu ya wananchi kujitokeza kushiriki na kushuhudia ngoma ya asili maarufu kama Mbina, iliyofanyika katika Mtaa wa Giriku, Kata ya Bunamhala, tarehe 21 Mei kama ilivyo kawaida kila mwaka.
Tukio hilo la kipekee limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Bariadi, OCD Jeronime Simon.
Mhe. Simalenga ameungana na wananchi katika kushiriki burudani hiyo ya kitamaduni, hatua inayoonesha kuthamini na kuendeleza urithi wa mila na desturi za jamii ya eneo hilo. Uwepo wake pamoja na viongozi wengine umeongeza chachu ya hamasa na mshikamano miongoni mwa wananchi waliohudhuria.
Ngoma ya Mbina imeendelea kuwa kivutio kikubwa cha kila mwaka, ambapo pamoja na burudani yake, pia huwakutanisha wananchi katika hali ya umoja, mshikamano na kujivunia utamaduni wao wa asili.
Mbali na tukio kuu, shughuli nyingine ndogo ndogo za kitamaduni hufanyika katika kata zote za Wilaya ya Bariadi, zikiwa na lengo la kuenzi na kuendeleza ngoma za asili pamoja na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Wananchi wamepongeza juhudi hizo zinazoendelea kuhuisha utamaduni, wakisisitiza kuwa matukio kama haya ni muhimu katika kulinda historia, maadili na mshikamano wa jamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mwisho.
0 Comments