Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU MWIGULU AINGILIA KATI UVUJAJI WA DAWA HOSPITALINI.





Na Kitoto Digital -Busega 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba, amevitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mnyororo wa usambazaji na utoaji wa dawa katika hospitali na vituo vya afya, ili kubaini mianya ya uvujaji wa dawa unaosababisha baadhi ya wagonjwa kulazimika kununua dawa nje ya vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, ameelekeza apewe taarifa kila mwezi kuhusu hali ya upatikanaji wa dawa na uwajibikaji wa watumishi wa sekta ya afya, akisisitiza kuwa hatakubali wananchi kuendelea kukosa huduma au kucheleweshewa matibabu kutokana na uzembe wa watumishi wa umma.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo, Novemba 8, 2026, katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Nyamikoma, wilayani Busega, mkoani Simiyu, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.



Amesema ni jambo lisilokubalika kwa mgonjwa anayefika hospitalini akiwa katika hali ya dharura, hususan mama mjamzito au majeruhi wa ajali, kucheleweshewa matibabu wakati maisha yake yanahitaji kuokolewa kwa haraka.

"Lazima tujue na tujali maisha ya wananchi na tusimamie mgawanyo wa dawa. Kila mkoa ninakopita napewa taarifa ya utoshelevu wa dawa kwenye hospitali na vituo vya afya kwa asilimia 96, lakini wagonjwa wananunua dawa nje. Nimeelekeza vyombo vya Ulinzi na Usalama kufuatilia mtiririko wa dawa ili tuimarisha utoaji wa huduma za afya," alisema.



Aliongeza kuwa serikali inataka kuona uwajibikaji katika kila ngazi ya utoaji wa huduma za afya, huku akiwataka watumishi wa umma kuwahudumia wananchi bila vikwazo na kuhakikisha wanaopata huduma katika ofisi za serikali hawalazimishwi kuwa na miadi maalumu, hasa kwa kuzingatia gharama wanazotumia kufika katika ofisi hizo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi, ikiwemo saruji, akisema serikali imetambua changamoto hiyo na imefuta kodi kwenye malighafi za saruji kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na kufanya bei ya bidhaa hiyo kuwa himilivu kwa wananchi.

Pia, aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa kutekeleza maelekezo yake ya kuwakutanisha wadau wa zao la pamba ili kujadili namna ya kurejesha mfumo wa soko huria, badala ya mfumo wa mnunuzi mmoja uliokuwa ukitumika awali.



Aliwataka wakulima kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji ili waweze kunufaika zaidi na kilimo cha pamba na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Awali, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Jafari Seif, alisema serikali imetenga Sh milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Lamadi, hatua inayolenga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.



Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Busega, Saimon Songe, alieleza kuwa Kata ya Kabita yenye wakazi takribani 36,000 bado haina kituo cha afya, hali inayosababisha changamoto kwa wananchi wanaohitaji huduma za matibabu.

Alisema tayari andiko la mradi wenye thamani ya Sh milioni 500 limewasilishwa serikalini kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ili kupunguza adha ya wananchi kufuata huduma za afya katika maeneo ya mbali.

Akizungumzia changamoto hiyo, mkazi wa wilaya hiyo, Catalina James, alisema bado kuna wagonjwa wanaocheleweshewa huduma wanapofika hospitalini katika hali zinazohitaji matibabu ya haraka, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha maisha yao.

"Ni kweli kuna wakati mgonjwa anafika hospitalini akiwa na hali mbaya lakini anachelewa kupata huduma, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha yake. Tunaiomba serikali isimamie agizo hili ili wagonjwa wahudumiwe kwa wakati bila kujali hali zao za kiuchumi," alisema.



Naye Josephat Daud alisema changamoto ya upatikanaji wa dawa katika baadhi ya vituo vya afya imekuwa ikiongeza gharama za matibabu kwa wananchi, kutokana na kulazimika kununua dawa nje ya hospitali.

Alisema hatua ya Waziri Mkuu kuagiza uchunguzi wa mtiririko wa dawa ni muhimu katika kuhakikisha dawa zinazotolewa na serikali zinawafikia walengwa na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi.

Kwa upande wake, Khija Seni alisisitiza umuhimu wa serikali kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa afya ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake ya msingi ya matibabu.

Alisema watumishi wanapaswa kutambua kuwa jukumu lao kubwa ni kuwahudumia wananchi, hivyo serikali inapaswa kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka wajibu wao na kusababisha wagonjwa kukosa huduma wanazostahili.

Mwisho.






Post a Comment

0 Comments