Na Kitoto Digital.
Mgogoro wa kimkataba kati ya wachimbaji wadogo wa madini katika Mgodi wa Ikibabushu, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, na mmiliki wa leseni ya uchimbaji madini anayefahamika kwa jina la Bonaventure, umefikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, baada ya wachimbaji hao kulalamikia ukiukwaji wa makubaliano waliyoingia.
Wachimbaji hao wamewasilisha malalamiko yao katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati wa siku maalumu ya Jumanne inayotumika kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Wakieleza chanzo cha mgogoro huo, wachimbaji hao wamesema hawaridhishwi na utekelezaji wa makubaliano ya mkataba waliouingia na mmiliki wa leseni, hali ambayo imesababisha kusimama kwa shughuli za uchimbaji na kuwaathiri kiuchumi.
Wameiomba Serikali kuingilia kati changamoto hiyo ili kuhakikisha haki zao zinapatikana na shughuli za uchimbaji zinaendelea kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Said mtandaoAkijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amesema amepokea malalamiko ya wachimbaji hao na kuahidi kumuita mmiliki wa leseni pamoja na wataalamu wake ili kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Mtanda amesema Serikali itasikiliza pande zote mbili kwa haki ili kubaini kiini cha mgogoro huo na kupata suluhisho litakalowezesha makubaliano ya mkataba kuzingatiwa na shughuli za uchimbaji kuendelea kwa utaratibu unaokubalika.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi wa Simiyu kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali wanapowasilisha malalamiko yao katika mamlaka husika, akieleza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kurahisisha upatikanaji wa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Mwisho.




0 Comments