Na Kitoto Digital - Maswa.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Chacha Maro, amewataka wanafunzi wa Chuo cha Maswa College of Health and Allied Sciences kutumia mitandao ya kijamii kwa malengo chanya, ikiwemo kujifunza na kuongeza uelewa wa masomo yao.
Akizungumza na wanafunzi hao, ACP Maro amesisitiza kuwa mitandao ya kijamii inapaswa kuwa nyenzo ya kuimarisha maarifa na kusaidia kufanikisha malengo yao ya kitaaluma badala ya kuitumia kwa shughuli zisizo na tija.
Aidha, amewaonya baadhi ya watumiaji wa mitandao wanaojihusisha na kusambaza taarifa za uongo, uchochezi na kutoa lugha zisizo za staha dhidi ya viongozi wa kisiasa na Serikali, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kuwa na athari za kisheria kwa mujibu wa sheria zinazosimamia matumizi ya mitandao.
Akisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya teknolojia hiyo, ACP Maro amesema, “Ninawasihi mtumie mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujifunza na kuongeza maarifa yatakayowasaidia kufikia malengo yenu, na si kuitumia kusambaza taarifa za uongo, uchochezi au lugha zisizo za staha.”
Elimu hiyo imetolewa Novemba 17, 2026 katika Chuo cha Maswa College of Health and Allied Sciences kilichopo Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu.
Mwisho.





0 Comments