Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

ONGEA NA KAMANDA: SUNGUSUNGU WATAKIWA KUPAMBANA NA UHALIFU SIMIYU.




Na Kitoto Digital.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Edith Swebe, amekutana na viongozi wa Sungusungu Wilaya ya Bariadi kupitia kampeni ya Ongea na Kamanda, inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kudumisha amani na usalama.


Kupitia kikao hicho, ACP Swebe amewataka viongozi hao kuwa chachu ya kupambana na uhalifu kwa kushirikiana na wananchi katika kuwabaini wahalifu na watu wachache wanaotaka kuvuruga amani katika jamii.


Akizungumza na viongozi hao, Swebe amesisitiza umuhimu wa Sungusungu kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za mapema kuhusu viashiria vya uhalifu ili hatua stahiki zichukuliwe kabla ya madhara kutokea.


“Viongozi wa Sungusungu mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia wananchi kuwabaini wahalifu na kuhakikisha watu wachache wenye nia ya kuvuruga amani wanadhibitiwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi,” amesisitiza Swebe.


Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Chacha Maro, amewataka viongozi wa Sungusungu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kusalimisha silaha haramu katika kipindi cha msamaha kinachoelekea ukingoni.


Maro amesema viongozi hao wana nafasi kubwa ya kuhamasisha wananchi wanaomiliki silaha haramu kuzisalimisha kwa mamlaka husika kabla ya muda wa msamaha kumalizika.


“Ninawasihi viongozi wa Sungusungu kutumia nafasi yenu kuhamasisha wananchi na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kusalimisha silaha haramu katika kipindi hiki cha msamaha, ambacho kimebakiwa na siku chache kabla ya kumalizika,” amesema Maro.


Ameongeza kuwa ushirikiano wa viongozi wa Sungusungu na wananchi ni muhimu katika kuzuia uhalifu, kudhibiti vitendo vinavyohatarisha usalama na kuhakikisha Mkoa wa Simiyu unaendelea kuwa na mazingira ya amani na utulivu.


Kampeni ya Ongea na Kamanda ni jukwaa linalowezesha Jeshi la Polisi kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usalama.

Mwisho.





Post a Comment

0 Comments