Na Kitoto Digital - Songwe.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kungu Kadogosa, amemuondoa katika nafasi yake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Songwe, Mhandisi Fredrick Mande, na kumtaka kurejea makao makuu ya wakala huo, kufuatia kushindwa kusimamia ipasavyo mradi wa ujenzi wa barabara ya Forodha–OSBP Tunduma, yenye urefu wa mita 1,675.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Waziri Kadogosa kufanya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo usiku wa Oktoba 15, 2026, ambapo alieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa kazi licha ya Serikali kutoa sehemu kubwa ya fedha za mradi huo.
Uamuzi huo umekuja kufuatia maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ambaye awali alieleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo inayopatikana katika mpaka wa Tanzania na Zambia.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Waziri Kadogosa alisisitiza umuhimu wa watendaji kuwajibika katika usimamizi wa miradi ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Kadogosa amempa mkandarasi anayetekeleza mradi huo muda wa wiki mbili kukamilisha kazi zilizobaki, akitaka kasi ya ujenzi iongezeke ili mradi ukamilike kwa wakati.
Aidha, Waziri huyo amesema atarejea eneo la mradi ndani ya siku saba zijazo kukagua maendeleo ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa na kujiridhisha kama mkandarasi amechukua hatua zinazostahili.
“Nitarejea hapa ndani ya siku saba kukagua utekelezaji wa maagizo niliyoyatoa na kujiridhisha kama kasi ya ujenzi imeongezeka,” amesema kadogosa.
Mradi huo ni muhimu katika kurahisisha shughuli za usafirishaji na biashara kati ya Tanzania na Zambia, kutokana na eneo la Tunduma kuwa kitovu muhimu cha biashara ya mipakani.
Hatua ya Waziri Kadogosa inatoa ujumbe kuhusu umuhimu wa uwajibikaji kwa viongozi na wakandarasi wanaopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali.
Je, mkandarasi ataweza kukamilisha kazi zilizobaki ndani ya muda aliopewa? Jibu linatarajiwa kujulikana katika siku zijazo, huku Waziri akiahidi kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake.🇹🇿🫣
Mwisho.





0 Comments