Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

SIMIYU YAWEKA ULINZI KABLA YA EL-NINO.

 



Na marykitoto. 

Katika kujiandaa kukabiliana na majanga yanayoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua kubwa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu limewajengea uwezo wanachama na volontia wa Red Cross kuhusu namna ya kukabiliana na moto na majanga mengine kwa usalama na weledi.


Mafunzo hayo yaliyofanyika leo Septemba 11, 2026, katika Ofisi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, yamekuja wakati mkoa huo ukiendelea kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa za El-Nino zinazotabiriwa kuanza mwezi Septemba.


Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustin Mtitu, amesema ushirikiano kati ya Jeshi hilo na Red Cross ni nguzo muhimu katika kuhakikisha jamii inakuwa tayari kukabiliana na majanga.

Tunapaswa kuendelea kuimarisha elimu ya kukabiliana na majanga na huduma ya kwanza kwa jamii zenye uhitaji, kabla, wakati na baada ya majanga.”



Mtitu amesema elimu hiyo itasaidia kuongeza uelewa na uwezo wa wananchi na wahudumu wa kujitolea kuchukua hatua sahihi wakati wa dharura, bila kuhatarisha maisha ya watu na mali.


Katika mafunzo hayo, washiriki wamepatiwa elimu kuhusu aina mbalimbali za moto, ikiwemo moto wa mimea, moto unaohusisha vyuma, gesi na vimiminika vinavyowaka.


Aidha, wamefundishwa mbinu salama za kuudhibiti moto na kuchukua hatua stahiki wakati wa dharura, kwa lengo la kuzuia madhara kwa raia na mali zao.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Red Cross Mkoa wa Simiyu, Sitta Tumma, amesema mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kuhakikisha jamii haikabili majanga ikiwa haijajiandaa.

Ni muhimu kujiandaa vizuri leo, ili kesho ufanye vizuri zaidi.”


Tumma amesema Red Cross Mkoa wa Simiyu, kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, itaendelea kuimarisha elimu ya kukabiliana na majanga pamoja na huduma ya kwanza kwa jamii nzima.

Mafunzo haya kwetu ni kielelezo cha mafanikio katika kuihudumia jamii kwa weledi,” amesema.



Kwa kuzingatia maandalizi kuelekea msimu wa mvua kubwa, wadau hao wameendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na uelewa wa msingi kuhusu namna ya kujikinga na majanga, kutoa msaada wa awali na kuwahi kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale tukio la dharura linapotokea.



Ushirikiano kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Red Cross unalenga kuhakikisha jamii ya Simiyu inakuwa na maarifa, utayari na uwezo wa kuchukua hatua sahihi wakati wa majanga, hivyo kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Ujumbe mkubwa kutoka katika mafunzo haya ni mmoja: Janga halisubiri maandalizi—jiandae kabla halijatokea.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments