Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

RC MTANDA ATOA KAULI NZITO SIMIYU: SINA CHAWA NIMEKUJA KUFANYA KAZI.

 



Na marykitoto. 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mohamed Mtanda, ameanza majukumu yake mkoani humo Septemba 4, 2026 na kutoa ujumbe mzito kwa viongozi, watumishi wa umma na wananchi, akisema amefika Simiyu kwa ajili ya kufanya kazi na kuharakisha maendeleo.


Mtanda, ambaye amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuongoza Simiyu, amesema anahitaji ushirikiano wa kila mmoja ili kuhakikisha changamoto za wananchi zinapatiwa majibu na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Nimekuja Simiyu kufanya kazi. Naomba ushirikiano katika shughuli za maendeleo. Kiongozi hapimwi kwa ukubwa wa eneo analoliongoza, bali kwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo.”



“Sina chawa, umri wa kuchaguliwa marafiki haupo”

Katika kauli iliyovuta hisia, Mtanda amesema hataki kujenga kundi la watu wanaomzunguka kwa maslahi binafsi, akisisitiza kuwa uongozi wake utazingatia kazi na maslahi ya wananchi.

“Niwahakikishieni mimi sina chawa. Umri wa kuchaguliwa marafiki kwa sasa haupo.”

Amesema anaamini katika uongozi unaozingatia utaratibu, uvumilivu na matokeo ya muda mrefu, badala ya kutafuta mafanikio ya haraka kupitia njia zisizo sahihi.

Mimi si mtu wa deal wala si mtu wa kutafuta deal. Ninaamini katika utendaji wa kazi. Nimechagua kula kidogo kidogo ila kwa muda mrefu.”


Asema yuko tayari kukosolewa

Mkuu huyo wa Mkoa amesema hatakuwa na tatizo kukosolewa au kujadiliwa kama kiongozi, akisisitiza kuwa mijadala inapaswa kujikita katika masuala yenye manufaa kwa jamii.

Ukiwa kiongozi ni lazima usemwe na ujadiliwe. Napenda watu wanaojadili mambo ya maana na si mtu.”



Amesema katika utumishi wake wa umma amejijenga katika misingi ya uwazi na kutokwamisha watu katika kutekeleza majukumu yao.

Katika utumishi wa umma mimi ni mtu muwazi, mkarimu na sipendi kukwamisha. Nafanya kazi bila kukwamisha.”


Rushwa na wizi wa fedha za umma hakuna nafasi

Mtanda amesema hatakuwa tayari kuvumilia wizi wa fedha za umma na vitendo vya rushwa, huku akitaka wananchi washirikishwe kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Wizi wa fedha mimi si mvumilivu, pamoja na vitendo vya rushwa. Tuwapatie wananchi nafasi.”



Amesema ushirikiano kati ya viongozi na watendaji ni muhimu, lakini hatakuwa tayari kutumia nguvu na muda wa Serikali katika mambo yasiyo na msingi.

Tufanye kazi kwa ushirikiano. Mimi siko tayari kufanyia kazi mambo ambayo hayana msingi.”


Wananchi waambiwa milango iko wazi

Katika kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kuwasilisha changamoto zao, Mtanda amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itakuwa wazi kwa wananchi bila kulazimika kupitia taratibu ngumu za kuomba miadi.

Nawahakikishia wananchi kuwa milango iko wazi kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Hakuna kuwekeana appointment.”

Amesema lengo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa sehemu ya mchakato wa kutafuta na kutekeleza suluhisho la changamoto zinazowakabili.


“Nikiachana na uongozi nitakaa vijijini”

Mtanda pia amesema maisha ya vijijini si mageni kwake, akieleza kuwa amezoea maisha hayo na ana mtazamo wa kuendelea kuyaishi hata baada ya kumaliza safari yake ya uongozi.

Nimezoea maisha ya kuishi vijijini na fikra zangu, nikiachana na uongozi nitakaa vijijini.”

Kauli hiyo inaendana na msisitizo wake wa kutaka viongozi kuwa karibu na wananchi na kuelewa hali halisi ya maisha yao.



Ampongeza DC Maswa kwa mpango wa madawati

Katika hatua nyingine, Mtanda amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Anney, kwa kuanzisha juhudi za kutengeneza madawati kwa ajili ya kupunguza tatizo la wanafunzi kukaa chini katika shule za wilaya hiyo.

Amesema juhudi hizo ni mfano wa mipango inayolenga kutatua changamoto halisi za wananchi na kwamba viongozi wanapaswa kuendelea kubuni mipango yenye matokeo yanayoonekana.



Mkuu huyo wa Mkoa amesema maendeleo ya Simiyu hayawezi kupatikana kwa juhudi za mtu mmoja, bali yanahitaji ushirikiano wa viongozi, watendaji wa Serikali na wananchi.

Ujumbe wake mkuu ni kwamba uongozi mpya unapaswa kupimwa kupitia matokeo ya kazi na maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi, badala ya ukubwa wa nafasi au mamlaka aliyonayo kiongozi.

Nimekuja Simiyu kufanya kazi. Naomba ushirikiano katika shughuli za maendeleo.”

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments