Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

MAGANYA ARIDHISHWA NA TACTICS BARIADI, ATOA MAELEKEZO.




Na marykitoto 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya, ameridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTICS) unaotekelezwa katika Mji wa Bariadi kwa gharama ya Sh bilioni 26.5.



Maganya amesisitiza umuhimu wa mradi huo kujengwa kwa ubora na kuzingatia viwango, huku akiwataka wahandisi na wakandarasi kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na wananchi wanaendelea kupata huduma bila usumbufu mkubwa.


Mradi huo unahusisha ujenzi wa Soko Kuu la Bariadi, barabara 13 za lami pamoja na jengo la wahandisi lenye maabara ya kisasa ya upimaji wa vifaa vya ujenzi.




Akizungumza wakati wa kukagua maendeleo ya mradi huo, Maganya amemtaka Mhandisi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuweka uangalizi wa karibu ili kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa mujibu wa viwango na muda uliopangwa.


Mhandisi wa Halmashauri uwe anafika na kuweka jicho lako hapa... mliyosema yafanyike ndani ya muda, msijifiche kwenye kichaka cha mvua,” alisema Maganya.



Aidha, Maganya amewataka wakandarasi kuhakikisha barabara zinazojengwa zinaendelezwa na kuwekwa katika hali inayowezesha wananchi kuzitumia wakati ujenzi ukiendelea. Amesisitiza pia umuhimu wa kutengeneza mitaro ya dharura na mifereji ya maji ili mvua zisiwe chanzo cha kuharibu miundombinu inayojengwa.



Kwa mujibu wa Mratibu wa Mradi huo, Mhandisi Hussein Katakweba, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 48, huku akibainisha kuwa mkandarasi yuko nyuma ya ratiba kwa takribani asilimia 14. Mradi unatarajiwa kukamilika Februari 2027.



Katakweba amesema ujenzi wa Soko Kuu pekee unagharimu takribani Sh bilioni 7, huku ujenzi wa barabara 13 na jengo la wahandisi ukigharimu Sh bilioni 19.5.


Mradi huo unatarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa miundombinu, mazingira ya biashara na shughuli za kiuchumi katika Mji wa Bariadi. Soko jipya litakuwa na maduka na vibanda vya kisasa kwa ajili ya wafanyabiashara.



Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, amesema wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika eneo la soko hilo wamezingatiwa katika mpango wa ugawaji wa vibanda baada ya ujenzi kukamilika, kwa kutumia taarifa zao zikiwemo namba za NIDA.



Mradi wa TACTICS unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya miji na kuchochea shughuli za kiuchumi, biashara na ustawi wa wananchi wa Bariadi.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments