Na marykitoto.
Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Simiyu kimegusa mioyo ya watoto wenye mahitaji maalum baada ya kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali katika kituo cha Bikira Maria Mama wa Mungu Msaada wa Daima, kilichopo Kata ya Lamadi, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Msaada huo umetolewa Agosti 30, 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi za kushirikiana na jamii pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya askari na wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Kikosi hicho, Mkufunzi Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Simiyu, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Amosi Lujiga, amesema msaada huo unaakisi dhamira ya Jeshi la Polisi ya kurudisha kwa jamii na kushiriki katika shughuli mbalimbali zenye manufaa kwa wananchi.
Amesema Jeshi la Polisi ni sehemu ya jamii, hivyo wananchi hawapaswi kuwa na hofu na Kikosi cha Kutuliza Ghasia, bali wanapaswa kuendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kutawala.
“Jeshi la Polisi ni sehemu ya jamii, hivyo wananchi hawana sababu ya kuwa na hofu na Kikosi cha Kutuliza Ghasia. Tunapaswa kushirikiana katika kulinda amani na usalama,” amesema ASP Lujiga.
Kwa upande wake, mlezi wa kituo hicho, Sister Maria Helena, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo, akisema vifaa vilivyotolewa vina umuhimu mkubwa katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Sister Maria Helena amesema msaada huo haujasaidia tu kupunguza changamoto zinazokikabili kituo, bali pia umekuwa faraja kubwa kwa watoto, ambao wanahitaji upendo, uangalizi na msaada kutoka kwa
Baada ya kukabidhi vifaa hivyo, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Simiyu walipata fursa ya kushiriki chakula cha pamoja na watoto wa kituo hicho.
Kitendo hicho kimeongeza uzito wa tukio hilo, kikionesha kuwa msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum hauishii kwenye vifaa pekee, bali pia unahusisha kujenga ukaribu, upendo na mshikamano kati ya jamii na watoto hao.
Zoezi hilo linaendelea kuonesha umuhimu wa taasisi za serikali kushirikiana na jamii katika kusaidia makundi yenye mahitaji maalum na kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya malezi na huduma.
Mwisho.
0 Comments