Na marykitoto.
Agosti 27, 2026. Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, amefanya ziara katika vijiji vya Mwasinasi, Mwaumatondo, Mwasilimbi na Ihusi, kwa lengo la kusikiliza kero zinazowakabili wananchi na kutoa maelekezo ya kuzitatua.
Katika ziara hiyo, wananchi walieleza changamoto mbalimbali, ikiwemo ubovu wa barabara unaochangiwa na mvua kubwa pamoja na uhaba wa maji, hali ambayo imekuwa ikiwalazimu baadhi ya wakazi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwasinasi, Talina Maduka, aliomba Serikali kuchukua hatua za haraka kurekebisha barabara zinazotumiwa na wananchi, akieleza kuwa hali hiyo imezidi kuwa mbaya kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
“Tunaiomba Serikali itusaidie katika urekebishaji wa barabara zetu, kwa sababu mvua kubwa zimezifanya ziwe katika hali mbaya. Pia upatikanaji wa maji bado hautoshelezi mahitaji ya wakazi wetu,” alisema Maduka.
Wananchi pia waliomba kupatiwa pampu za mkono kwa ajili ya visima vilivyopo, ili kuwawezesha kupata maji wakati wakisubiri utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji.
Mhandisi Nusra Msoke, kutoka Ofisi ya RUWASA, Meneja wa Bariadi, alikiri kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo hayo.
Alieleza kuwa suluhisho la muda ni kuimarisha matumizi ya visima vilivyopo kwa kuvifungia pampu za mkono.
“Tunatambua changamoto ya upungufu wa maji iliyopo. Tunaomba uongozi kupitia Mtendaji wa Kata kuandika barua kwa Meneja wa RUWASA Bariadi kuomba pampu za mkono, ili kutosheleza visima vilivyopo wakati wananchi wakisubiri mradi mkubwa wa maji,” alisema Mhandisi
Kwa upande wake, Mhandisi Musa Hald, aliomba radhi kwa wananchi kutokana na adha wanayoipata kutokana na hali mbaya ya barabara, akieleza kuwa tayari TARURA imeanza kuchukua hatua.
“Tunaomba radhi kwa kadhia ambayo wananchi wanapitia. TARURA tayari imezungumza na Mkandarasi na kuanzia Jumatano ataanza kazi,” alisema Mhandisi Hald.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, hakuridhishwa na hali ya barabara alizoziona wakati wa ziara hiyo, akieleza kuwa wananchi wamekuwa wakikumbana na changamoto kubwa kutokana na miundombinu hiyo.
Akaagiza hatua za haraka kuchukuliwa, huku akimtaka Mkandarasi kuhakikisha anafika katika maeneo husika na kuanza utekelezaji wa ukarabati.
“Kuanzia Jumatatu, Mkandarasi anatakiwa awe site. Hatutaki kuona wananchi wakiendelea kuteseka kwa sababu ya barabara hizi na makaravati yaliyoharibika,” alisema Mhe. Simalenga.
Mbali na changamoto za barabara na maji, Mhe. Simalenga aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na utabiri wa uwezekano wa mvua kubwa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Aliwasihi wananchi kujenga utamaduni wa kuhifadhi chakula mapema, ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza endapo mvua hizo zitasababisha usumbufu wa shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Wananchi tunapaswa kuwa tayari. Tunashauriwa kuhifadhi chakula kwa tahadhari kwa sababu utabiri unaonyesha uwezekano wa mvua kubwa. Ni muhimu kuchukua tahadhari mapema kuliko kusubiri madhara yatokee,” alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Simalenga aliwataka wazazi na walimu kuwa walinzi wa watoto na wanafunzi, hususan wakati wa mvua kubwa.
Aliwataka kuhakikisha watoto wanapewa elimu ya kutosha kuhusu madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko na maeneo yenye maji mengi, huku akisisitiza kuwa watoto wasiruhusiwe kuvuka maeneo hatarishi.
“Wazazi na walimu muwe walinzi wa watoto wetu. Mvua ikinyesha kwa kiwango kikubwa, msiruhusu watoto kuvuka maeneo yenye maji mengi au maeneo mengine hatarishi. Usalama wa mtoto ni jukumu letu sote,” alisema.
Ziara hiyo imeweka msisitizo katika utatuzi wa changamoto za barabara na maji, huku viongozi wa Serikali wakiahidi kuchukua hatua za haraka ili kuboresha huduma na mazingira ya wananchi katika maeneo hayo.
Mwisho.
0 Comments